array(0) { } Radio Maisha | Hatuna Mshambulizi Hodari, Kauli ya kocha wa Kariobangi Sharks William Muluya

Hatuna Mshambulizi Hodari, Kauli ya kocha wa Kariobangi Sharks William Muluya

Hatuna Mshambulizi Hodari, Kauli ya kocha wa Kariobangi Sharks William Muluya

Mapema Alhamisi, Mkufunzi wa klabu ya Kariobangi Sharks fc amelalamikia idara yake ya ushambuliaji, na kuitaja kuwa tepetevu.

Akizungumza katika kikao maalum na idara ya michezo Redio Maisha kutoka uwanja wa Camp Toyoyo, kocha huyo almaarufu kama 'Kanu' mitaani alisisitiza ya kwamba bado Kariobangi Sharks itawania taji la ligii kuu nchini KPL na ngao.

“Ndio lengo letu haswa baada ya kudhihirishia ulimwengu wa soka nchini Kenya ya kwamba tunaweza, ubingwa wa ligii kuu KPL ni ndoto yetu sasa, hatutaki pia tusubiri sana maanake mla ni mla leo, ni kweli kwamba tumeanza vibaya msimu huu, lakini bado tuna mechi zaidi ya 28 na  nina imani vijana wangu wanaboreka kila uchao.”

Muluya alijipa matumaini huku akiongeza kwamba msimu huu hakuna yule atakaye kosa kula kichapo.

Klabu hiyo ambayo ilibuniwa mwaka 2000, katika vitongoji duni vya mtaa wa Kariobangi  Nairobi. Ilishiriki mara ya kwanza katika ligi ya KPL msimu wa mwaka 2016/2017.

Mwaka wa 2018, mambo yaliwaendea sambamba walipotoka nyuma na kuwatandika vigogo Sofapaka mabao matatu kwa mawili katika fainali za taji la ngao nchini.

“ Tulianza vizuri na tumekuwa tukiendelea vizuri lakini hakuna ufanisi bila changamoto, kwa sasa ushambuliaji wetu hauna makali na nafasi tunazozibuni lakini hatuna mmaliziaji hodari."

Alinung’unika Muluya, huku akiwaonya vikali wachezaji wake katika safu ya ushambulizi  kwamba iwapo hawatafanya vyema basi wakumbuke shoka la mchujo nalo haliko mbali.

Mwaka wa 2017, aliyekuwa mshambuliaji wa klabu hiyo Masoud Juma alimaliza mfungaji bora katika ligii ya  KPL kwa idadi ya magoli 17 hulu K-sharks ikimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Sofapaka na mabingwa wa ligi ya KPL Gormahia.

Mwaka 2018, klabu hiyo ya mtaani Kariobangi ambayo inamilikiwa na rais wa shirikisho la soka FKF Nick Mwendwa, ilitoa mfungaji bora na pia mchezaji bora wa msimu huo.

Erick Kapaito, alifungia K-Sharks mabao 16 msimu huo na kumaliza mfungaji bora wa ligii kuu nchini KPL.

Sharks msimu huo walimaliza katika nafasi ya sita kwenye jedwali ya ligi ya Kpl. Kwa sasa vijana hao wa Muluya wako katika nafasi ya 15 kwa alama 7 baada ya kucheza mechi nane.

Gumzo kubwa mitaani kwa sasa, ni kuhusu maswala ambayo yanawatatiza vijana hao  katika mtaa wa Kariobangi, lakini wazingatie ya kwamba heri kuanza vibaya umalize vizuri kuliko kuanza vizuri kisha umalize vibaya.