array(0) { } Radio Maisha | Mwanawe Akasha kuhukumiwa Ijumaa Marekani

Mwanawe Akasha kuhukumiwa Ijumaa Marekani

Mwanawe Akasha kuhukumiwa Ijumaa Marekani

Na Sam Amani,

NAIROBI, KENYA, Ibrahim Akasha ambaye ni nduguye mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa mihadarati Baktash Akasha anatarajia kujua hatma yake Ijumaa hii, wakati ambapo mahakama moja jijini New York, Marekani itakapotoa uamuzi kuhusu kesi inayomhusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mahakama hiyo itatoa uamuzi huo miezi mitatu tu baada ya Baktash Akasha kuhukumiwa miaka ishirini na mitano gerezani.

Uamuzi wa leo aidha unafasiriwa kuwa huenda ukasitisha mtandao wa ulanguzi wa  dawa za kulevya duniani  hasa ikizingatiwa kuwa babayao aliuliwa kwa kupigwa risasi jijini Amsterdam nchini Uholanzi  akihusishwa na ulanguzi wa mihadarati.

Ibrahim alikiri mashtaka yanayohusiana na biashara hiyo haramu kukiwamo kuwahonga maafisa wakuu katika serikali ya Kenya ili kuendesha biashara yake bila vikwazo.

Ikumbukwe walipokabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Mombasa humu nchini, Ibrahim na nduguye Baktash waliomba mahakama kuwa kifungo kifupi wakisema wangeteseka iwapo watafungwa jela kwa muda mrefu kabla ya wawili hao kufunguliwa mashtaka nchini Marekani.

Mwezi Agosti mwaka huu, Jaji Victor Marrero alitoa hukumu ya miaka ishirini na mitano gerezani kwa Baktash huku akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni kumi nukta tatu pesa za Kenya.