array(0) { } Radio Maisha | Imran Okoth atangazwa mshindi Kibra

Imran Okoth atangazwa mshindi Kibra

Imran Okoth atangazwa mshindi Kibra

Na Mate Tongola,

NAIROBI, KENYA, Tume ya IEBC imetangaza Imran Okoth kuwa Mbunge Mteule wa Eneo Bunge la Kibra.

Afisa Msimamizi wa uchaguzi huo kwenye eneo la Kibra, Beatrice Muli anaongoza shughuli hiyo. Okoth amepata jumla ya kura elfu ishirini na nne mia sita thelathini na sita. 

MacDonald Mariga wa Jubilee ni wa pili akiwa na jumla ya kura elfu kumi na moja mia mbili thelathini huku Eliud Owalo wa ANC akiwa wa tatu kwa kura elfu tano mia mbili sabini na tano.

Muli amewapongeza wagombea wote ishirini na wanne walioshiriki uchaguzi huo mdogo kwa kukubali matokeo. Aidha, amesema ni jumla ya wapigakura elfu arubaini na mbili na thelathini na saba waliojitokeza miongoni mwa zaidi ya laki moja waliosajiliwa ikiwa ni asilimia 35.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Chama cha Jubilee ambao walikuwa maajenti kwenye uchaguzi huo wamesisitiza kuwa licha ya kushindwa, wamefanya vizuri katika uchaguzi huo  na kwamba kinyang'anyiro kikali kitakuwa mwaka 2022.

Katika uchaguzi huo visa mbalimbali viliripotiwa wakati wa shughuli hiyo hapo jana, yakiwamo madai ya udanganyifu huku idadi ndogo zaidi ya wapigakura wakijitokeza kushiriki. Washukiwa watatu walikamatwa kwa kuhusishwa na udanganyifu huo, huku watu wawili wakijeruhiwa wakati wa virugu zilizoshuhudiwa katika kituo cha kupigia kura cha Mashimoni.