array(0) { } Radio Maisha | Waziri George Magoha aonya kuhusu udanganyifu katika KCSE

Waziri George Magoha aonya kuhusu udanganyifu katika KCSE

Waziri George Magoha aonya kuhusu udanganyifu katika KCSE

Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha amesema kuwa takriban watu saba wametiwa nguvuni na polisi wakijifanya watahiniwa wa Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne, KSCE katika shule moja ya binafisi katika Kaunti ya Kisii.

Washukiwa wamenaswa pamoja na mmiliki wa shule hiyo na watu wengine wanne ambao watafikishwa mahakamani kesho ili kufunguliwa mashtaka.

Magoha amesema mpango wao ulikuwa kufaulisha udanganyifu wa mitihani katika eneo la Nyanza ambapo amekita kambi kuanzia jana kukagua shughuli hiyo. Waziri Magoha kwa mara nyingine amewaonya walimu na maafisa wa mitihani hiyo dhidi ya udanganyifu.

Amesema serikali inafahamu njama ya baadhi ya wazazi katika Kaunti za Homa Bay, Migori na Kisiii ambao wanashirikiana na wasimamizi na polisi kufanikisha udanganyifu wa mitihani hiyo huku akisema wanafuatiliwa kwa karibu.

Msimamizi mmoja wa KCSE, amefikishwa leo mahakamani baada ya kunaswa jana kwenye eneo la Nairobi West kwa kufungua karatasi ya mitihani kabla ya wakati uliostahili.

Haya yanajiri wakati ambapo wanafunzi ishirini na mmoja ambao hawakuhudhuria masomo wamejitokeza kuufanya mtihani huo katika eneo Bunge la Mugirango Kusini.