array(0) { } Radio Maisha | Aisha Jumwa amekamatwa
Aisha Jumwa amekamatwa

Polisi wamethibitisha kumkamata Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa nyumbani kwake kwenye neo la Kakuyuni kwa kuhusishwa na kisa ambapo mtu mmoja aliuliwa kwa kupigiwa risasi eneo la Ganda, Kaunti ya Kilifi.

Jumwa anatarajiwa kuhojiwa kufuatia tukio hilo ambalo lilitokea katika boma la mmoja wa wagombea wa wadhifa wa Uwakilishi Wadi katika Wadi ya Ganda kwa tiketi ya chama cha ODM, Reuben Katana.

Awali, Jumwa alikanusha taarifa za kukamatwa kwake akisisitiza kwamba hakuwa na kosa lolote.

Rabsha hizo zilizuka baada ya Jumwa kuvamia boma hilo kwa kile kinachodaiwa kuwa kulenga kutatiza mkutano uliokuwa ukiendelea baina ya Katana na maajenti wa ODM kupanga mikakati ya uchaguzi mdogo wa wadi hiyo utakaofanyika kesho.

Waliokuwepo wanadai kwamba Jumwa aliwasili katika boma hilo akisema kwamba mkutano huo haukuwa halali kwani muda wa kuendesha kampeni ulikuwa umekamilika kwa mujibu wa sheria za Tume ya Uchanguzi, IEBC.

Ikumbukwe kuwa Jumwa ambaye ametangaza hadharani kuunga mkono azma ya Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022, amekuwa akimpigia debe Abdul Omar, mgombea huru katika uchaguzi huo mdogo uliotangazwa na IEBC kufuatia kufutiliwa mbali kwa uchaguzi wa Abdulrahman Omar.