array(0) { } Radio Maisha | Pigo kwa Mswada wa Punguza Mizigo

Pigo kwa Mswada wa Punguza Mizigo

Pigo kwa Mswada wa Punguza Mizigo

Na Sammy Amani,

NAIROBI, KENYA, Huku Mswada wa Punguza Mizigo ukiendelea kuangushwa kwenye mabunge ya Kaunti mbalimbali, Bunge la Kuanti ya Kajiado limethibitisha kuupokea mswada huo na kwa sasa unatathiminiwa na kamati ya Sheria.

Katika tangazo kwa umma Karani wa Bunge hilo Leboo Saisa amewataka wananchi walio na hoja kuziwasilisha kufikia Jumatatu saa kumi na moja jioni kabla ya mswada huo kujadiliwa bungeni.

Kufikia sasa mabunge kumi na matano ya kaunti, yameuangusha mswada huo. Mabunge hayo ni Tharaka Nithi, Nyeri,  Nairobi, Kirinyaga, Nakuru, Makueni, Murang'a, Homa Bay, Siaya, Nyamira, Kisii, Narok, Kiambu, Pokot Magharibi na Machakos.

Bunge la Uasin Gishu ndilo la pekee ambalo limeupitisha mswada huo.

Licha ya hayo Kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance Dkt. Ekuru Aukot, amesema ataendelea kuupigia debe mswada huo hadi utakapoidhinishwa na mabunge ishirini na manne inavyohitajika kisheria.

Wakati uo huo, ameendelea kuwashtumu wanasiasa anaodai wameyachochea mabunge ya kaunti kuuangusha.

Ili mswada huo uiidhinishwe unahitaji kupitishwa kwa angalau mabunge ishirini na manne miongoni mwa arubaini yote na saba.