array(0) { } Radio Maisha | Gari lililozama Likoni kuopolewa Alhamisi

Gari lililozama Likoni kuopolewa Alhamisi

Gari lililozama Likoni kuopolewa Alhamisi

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Shughuli ya kulitoa gari lililozama katika Kivuko cha Likoni likiwa na Mariam Kigenda na mwanawe Amanda Mutheu inatarajiwa kufanyika Alhamisi kuanzia saa tatu asubuhi.

Kutolewa kwa gari hilo kunajiri baada ya Maafisa wa Jeshi la Wanamaji na wapiga-mbizi wa binafsi kuendesha shughuli ya kulitafuta gari hilo kwa takribani siku kumi na moja.

Msemaji wa Serikali Kanali Mustaafu Cyrus Oguna alithibitisha jana jioni kwamba gari hilo aina ya Toyota ISIS lenye namba ya usajili ya KCB 289C lilionekana katika kina cha mita hamsini na nane katika kivuko hicho. Alisema kamera maalum za 3HD zilitumika katika kunasa picha za gari hilo.

Aidha, Oguna alisema kwamba hawana uhakika wa asilimia mia moja iwapo mili ya wawili hao ingali ndani ya gari hilo na hivyo kuwashauri wananchi kuwa na subra, akisema watabaini iwapo mili hiyo iko ndani ya gari hilo baada ya kulitoa leo. Hata hivyo ameeleza matumaini ya kuipata mili hiyo katika gari hilo.

Wakati uo huo, familia ya Mariam ikiongozwa na Stephen Kayoki wameipongeza serikali na vitengo mbalimbali vinnavyoshirikishwa katika kufanikisha shughuli ya kuiopoa mili ya wapendwa wao.

Kighenda na mwanawe walizama baharini tarehe 29 mwezi uliopita baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye Feri MV. Harambee.