array(0) { } Radio Maisha | Mapya kuhusu kesi ya Mgao wa Fedha za Kaunti

Mapya kuhusu kesi ya Mgao wa Fedha za Kaunti

Mapya kuhusu kesi ya Mgao wa Fedha za Kaunti

Mahakama ya Juu itaendelea kusikiza kesi inahusu Mgao wa Fedha za kaunti kwa kuzingatia sheria.

Ndiyo kauli ya Jaji Njoki Ndung'u katika Mahakama ya Juu leo hii ambapo ametupilia mbali kesi ya Bunge la Kitaifa ambayo ililenga kupinga hatua ya magavana kutafuta usaidizi wa mahakama kufuatia mgogoro wa mgao huo wa fedha kutokaa kwa serikali ya kitaifa.

Akitoa uamuzi kuhusu hatua ya Baraza la Magavana kutaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu ni nani anafaa kuamua kiwango cha fedha za kaunti kutoka kwa serikali ya kitaifa, Jaji Ndung'u amesema Mahakama ya Juu itashughulikia masuala manne pekee miongoni mwa kumi na mawili yaliyowasilishwa na magavana kuhusu suala hilo.

Amesema masuala hayo manne yanahusu kesi kadhaa ambazo zinasubiri kuamuliwa kwenye mahakama kuu.

Masuala yatakayoshughulikiwa na mahakama hiyo yatabainishwa kwa wanaohusika katika kesi hiyo kupitia mawakili wao.

Bunge la Kitaifa liliwasilisha kesi hiyo mahakamani kupinga hatua ya viongozi wa kaunti wakiwamo magavana, kuwasilisha kesi mahakamali ili kupata mwelekeo kufuatia mgogoro baina ya Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kuhusu mgao huo.

Ikumbukwe kesi sawa na hiyo iliwasilishwa Katika Mahakama ya Juu mwaka 2013, ambapo aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga alitoa ushauri kwamba bunge la kitaifa, seneti na magavana wanafaa kushauriana kuhusu kiwango cha mgao wa fedha za kaunti kabla ya miswada ya mgao huo kuwasilishwa bungeni ili kuepuka mivutano.