array(0) { } Radio Maisha | Wapiga mbizi kutoka Afrika Kusini kuwasili Likoni

Wapiga mbizi kutoka Afrika Kusini kuwasili Likoni

Wapiga mbizi kutoka Afrika Kusini kuwasili Likoni

Jumla ya maeneo kumi miongoni mwa kumi na manne yanayokisiwa huenda gari lilikuwa na watu waliozama katika Kivuko cha Likoni lilikwama yamefanyiwa ukaguzi bila mafanikio.

Msemaji wa Serikali Kanali Mstaafu Cyrus Oguna amesema kwamba tangu jana wapiga-mbizi wamekuwa wakiendelea kuyakagua maeneo manne yaliyosalia ambayo ni ya kina kirefu.

Amesema kwamba leo wapiga-mbizi hao watafanya ukaguzi kwenye maeneo mawili miongoni mwa manne hayo.

Amesema kwamba urefu wa kina wa maeneo hayo ni hatari kwa wapiga-mbizi huku wakilazimika kupiga mbizi kwa dakika sita pekee ikilinganishwa na awali.

Amewahimiza Wakenya kuwa na subra ili wakati huu ambao oparesheni ya kuitafuta mili ya Mariam Kigenda na mwanawe Amanda Mutheu inaendelea.

Akizungumzia suala la Mamlaka ya Bandari ya Mombasa kukiuka agizo lililotolewa jana na Mjumbe Maalum wa Masuala ya Muundo Msingi Afrika Raila Odinga la kuistishwa kwa uchimbaji mchanga baharini, Oguna amesema kwamba mazungumzo ya kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa yanaendelezwa.

Kuhusu wapiga-mbizi kutoka Afrika Kusini ambao wamekodishwa na familia ya Mariam na Amanda, Oguna amesema kwamba kikosi cha kwanza kitafika leo huku kingine kikiwasili kesho kisha kufanya mazungumzo na mkuu wa oparesheni hiyo Lawrence Gituma kabla kujumuika na wapiga-mbizi wa humu nchini jumanne.

Ikumbukwe aliagiza kusitisha kwa shughuli ya uchimbaji na uondoaji mchanga japo limeonekana kupuuzwakwani shughuli hiyo imeendelezwa leo.