array(0) { } Radio Maisha | Serikali kutafuta suluhu ya mzozo wa Ardhi Isiolo

Serikali kutafuta suluhu ya mzozo wa Ardhi Isiolo

Serikali kutafuta suluhu ya mzozo wa Ardhi Isiolo

Serikali ya Kitaifa na ile ya Kaunti ya Isiolo zimetakiwa kutafuta njia mwafaka ya kusuluhisha mzozo wa ardhi katika Wadi ya Burat baina ya wakazi na Maafisa wa Jeshi la Ulinzi KDF.

Wakizungumza na wanahabari mjini Isiolo, viongozi wa makanisa katika kaunti hiyo wameiomba serikali kusitisha hati ya makataa ya mwezi mmoja inayowataka wakazi hao kuondoka kwenye kipande hicho cha ardi, ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa mazungumzo ya kusaka suluhu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Wachungaji katika Kaunti ya Isiolo Solomon Kinyua, mzozo huo unapaswa kutatuliwa kwa njia ambayo haitawaathiri wakazi, wakisema kwamba wakazi hao wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kwa miongo kadhaa kabla ya Jeshi la KDF kugawiwa sehemu ya ardhi hiyo.

Kwenye kikao na wananahabari mjini Isiolo, aidha Katibu wa Muungano wa Wachungaji katika kaunti hiyo David Nzioka amesema iwapo wakazi hao watalazimishwa kulihama eneo hilo, zaidi ya watu elfu ishirini wataathirika. Amesema kwamba tayari serikali imewekeza katika Sketa ya Elimu kwa kujenga shule mbili za upili, nane za msingi , vituo viwili vya afya vilevile miradi kadhaa ya maji katika eneo hilo, ishara kwamba wakazi hao wana haki ya kuendelea kuishi katika eneo hilo.

Miongoni mwa maeneo ambayo yataathirika na makataa hayo ni Elsa Ntirim, Akadeli, Kakili, Ngisoro, Blues Dima na Leparua, yote yakiwa katika Wadi ya Burat.