array(0) { } Radio Maisha | Mkewe Daktari Bonny Khalwale, Adelaide Khalwale afariki

Mkewe Daktari Bonny Khalwale, Adelaide Khalwale afariki

Mkewe Daktari Bonny Khalwale, Adelaide Khalwale afariki

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Bonni Khalwale amesema mkewe wa kwanza, Adelaide Khalwale amefariki kufuatia ugonjwa wa Shinikizo la Damu linaloathiri Mishipa ya Moyo na Mapafu, Pulmonary Hypertension wala si ugonjwa wa saratani jinsi ilivyodaiwa awali.

Akizungumza nyumbani kwake katika eneo la Malinya Kaunti ya Kakamega, Khalwale hata hivyo amesema mkewe alipata ugonjwa saratani njia ya uzazi, Cervical Cancer mwaka wa 2003  na kutibiwa kupitia Chemotherapy.

Aidha, amesema mapema mwaka huu, alipata saratani ya damu, Multiple Myloma lakini akafaulu kupata matibabu kwa wakati.

Khalwale  amewapongeza madaktari wote waliohakikisha mkewe anapata matibabu. Aidha ameupongeza usimamizi  wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro alikofanya kazi mkewe kwa kumsaidia.

Amesema viongozi mbalimbali akiwamo Naibu wa Rais, William Ruto wametuma risala za rambirambi kwa familia yake.

Wakati uo huo, Khalwale amesema shughuli za mazishi zitaanza punde tu kakaye mkubwa atakapotoa mwelekeo kwani kulingana na mila na desturi za Jamii ya Mulembe, haruhusiwi kutoa mwelekeo wowote kwa sasa.

Mkewe amefariki mapema leo huku mwili wake ukihifadhiwa katika Chumba cha Maiti cha Mukumu.