array(0) { } Radio Maisha | Waititu atetewa baada ya kuorodheshwa nambari 47 katika ripoti ya AAA

Waititu atetewa baada ya kuorodheshwa nambari 47 katika ripoti ya AAA

Waititu atetewa baada ya kuorodheshwa nambari 47 katika ripoti ya AAA

Bara za Magavana limepuuza utafiti uliomworodhesha Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu kuwa wa mwisho katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa baraza hilo, Wycliffe Oparanya ametilia shaka utafiti huo, akisema unalenga kuwadhalilisha magavana.

Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, aidha amesema magavana wala wakazi katika kaunti zote arubaini na saba hawakuhusishwa.

Gavana Oparanya ameitaja ripoti hiyo iliyofanywa na Taasisi ya All Afrika Advisory, AAA kuwa ya kisiasa na wakuu wake wanatumiwa na watu Fulani kuwadhalilisha magavana.

Amesema miradi katika kaunti mbalimbali haziwezi kulinganishwa hasa ikizingatiwa kila kaunti ina miradi yake iliyofanywa kipaumbele.

Mwenyekiti huyo ameitaka AAA kuwaomba msamaha magavana la sivyo wakuu wake watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuendesha utafiti unaoegemea upande mmoja.

Ikumbukwe utafiti huo ulimworodhesha Gavana Alfred Mutua wa Machakos kuwa nambari moja, akifuatwa na Oparanya, Gavana Mike Sonko wa Nairobi namba tatu, Kivutha Kibwana nambari nne na Ali Hassan Joho wa Mombasa kuwa nambari tano.

Magavana watano walioshikilia mkia ni pamoja na Amoson Jeffa Kingi wa Kilifi nambari 43, Fahim Twaha wa Lamu namba 44, Sospeter Ojamong Busia nambari 45, Cyprian Owiti wa Homa Bay nambari 46 kisha Gavana Waititu wa Kiambu kushikilia mkia kwa nambari 47 juu ya 47.