array(0) { } Radio Maisha | Baraza La Magavana lamkosoa Waziri Yattani

Baraza La Magavana lamkosoa Waziri Yattani

Baraza La Magavana lamkosoa Waziri Yattani

Baraza la Magavana limesema magavana hawajapokea fedha zozote, licha ya Wizara ya Fedha kusema imetoa shilingi bilioni 50, ili kukwamua shughuli za kaunti baada ya Rais Kenyatta kutia saini Mswada wa Ugavi wa Mapato.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa baraza hilo Wycliif Oparanya, amemkosoa Kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yattani kwa kuupotosha umma siku iliyopita, katika taarifa yake ya kusema fedha zimetumwa kwa serikali za kaunti.

Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kakamega amesema Waziri Yattani alifaa kuthibitisha iwapo kweli fedha hizo zilikuwa zimetumwa kabla ya kuwatubia wanahabari.

Oparanya vilevile amemlaumu Yattani kwa kuwadanganya Wakenya huku akidai taarifa yake imewafanya wananchi kutilia shaka utendakazi wa magavana.

Kwenye tangazo lake Waziri Yattani alisema shilingi bilioni 50 zilikuwa zimetumwa kwa akaunti za serikali za kaunti ili kughamikia shughuli za mwezi Julai na Agosti.