array(0) { } Radio Maisha | Mkewe mfanyabiashara Tob Cohen kuendelea kuzuiliwa

Mkewe mfanyabiashara Tob Cohen kuendelea kuzuiliwa

Mkewe mfanyabiashara Tob Cohen kuendelea kuzuiliwa

Mkewe mfanyabiashara Tob Cohen aliyeuliwa kisha mwili kutupwa katika tenki la maji nyumbani kwake, Sara Wairimu Cohen ataendelea kuzuiliwa kwa muda wa siku kumi ili kutoa nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kesi hiyo kuendelea tarehe 26 mwezi huu.

Wairimu amefikishwa katika Mahakama ya Milimani mapema leo katika kikao cha kwanza cha kesi ambayo ametajwa kuwa mhusika kuu katika mauaji ya Cohen.

Wairimu kupitia wakili wake Philip Murgor aidha amewasilisha ombi la kutaka mteja wake kuachiliwa kwa dhamana akisema amekuwa akizuiliwa kwa takribani siku ishirini bila ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Jaji Jessie Lessit aidha ametoa muda wa wiki mbili kwa Wairimu kuhakikisha anafanyiwa uchuguzi wa kiasili kabla ya kurejeshwa mahakamani wiki ijayo kujua hatma ya ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Akitoa maagizo ya namna vikao vya kesi hiyo vitakavyoendeshwa, Jaji Lessit amezizuia pande zinazohusika katika kesi hiyo ukiwamo upande wa utetezi, upande wa mashtaka na Idara ya Upelezi DCI kutozungumzia mchakato wa uchuguzi wa kifo cha Cohen katika vyombo vya habari.

Lessit aidha ameviagiza vyombo vya habari kutochapisha taarifa yoyote kuhusu uchunguzi unaoendelea katika kesi hiyo jinsi alivyozikataza pande zinazohusika kuwahutubia wanahabari kuhusu suala lolote katika kesi hiyo.

Kuhusu suala la upasuaji wa mwili wa Cohen, Wakili Murgor ameiambia mahakama kwamba maafisa wa polisi wanapania kubaini kilichosababisha mauaji yake na kwamba waliomba kuahirisha shughuli ya upasuaji hadi Jumanne wiki ijayo saa tatu asubuhi, kinyume na ilivyoratibiwa kuwa leo saa nane mchana.

Wakili Wyclif Ombeta ambaye ameiwakilisha familia ya marehemu Cohen amesema watapinga hatua ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka Wairimu kuachiliwa kwa dhamana.

Wairimu amekuwa akizuiliwa tangu tarehe 28 mwezi Agosti baada ya kakamatwa akihusishwa na kutoweka kwa mumewe Tob Cohen ambaye baadaye alipatikana akiwa ameuliwa.