array(0) { } Radio Maisha | Murgor amepuuzilia mbali madai kwamba mteja wake alihusika katika mauaji ya mumewe

Murgor amepuuzilia mbali madai kwamba mteja wake alihusika katika mauaji ya mumewe

Murgor amepuuzilia mbali madai kwamba mteja wake alihusika katika mauaji ya mumewe

Wakili wa Sarah Wairimu Cohen, Philip Murgor amepuuzilia mbali madai kwamba mteja wake alihusika katika mauaji ya mumewe Tob Cohen ambaye mwili wake ulipatikana katika tenki la maji-taka jana.

Akizungumza siku moja tu baada ya mwili wa Cohen kupatikana nyumbani kwake mtaani Kitisuru Kaunti ya Kiambu, Murgor amesema mteja wake amekuwa akizuiliwa kwa siku kumi na saba gerezani hivyo hangeweza kutekeleza mauaji dhidi ya mumewe. Aidha amesema Kinoti na maafisa wake waliandamana na Sarah hadi nyumbani kwake ambapo aliruhusiwa kuoga vilevile kubadilisha nguo huku msako ukiendeshwa chumbani humo.

Amesema inashangaza kuona kwamba mwili huo ulipatikana katika tenki hilo ilhali walikuwa wameangalia awali na hawakuupata. Aidha ameibua madai kuwa maafisa hao waliwalazimisha wafanyakazi wa Cohen kusalia chumbani usiku wa Jumanne wiki hii baada ya Sarah kuwapa funguo.

Vilevile Murgor amesema maafisa hao hawakufanya msako mbele ya mawakili wa Sarah wala walinzi waliokuwa wamejukumiwa kulinda boma hilo.

Wakati uo huo, Murgor amemshtumu Kinoti kwa kutaja boma la mteja wake kuwa eneo la mauaji hivyo hakuna aliyeruhusiwa kuingia.

Kauli yake inajiri siku moja tu baada ya Kinoti kusisitiza kwamba uchunguzi utaendelea licha ya pingamizi kutoka kwa wakili huyo.

Tayari washukiwa wawili akiwamo Peter Karanja aliyekuwa mumewe Mbunge wa Gilgil, Martha Wangari wamekamatwa huku wengine wanne wakitafutwa.

Kinoti amesema afisi yake imepokea taarifa muhimu kuhusu mauaji hayo huku uchunguzi wa awali ukibainisha kuwa washukiwa walipokea fedha shilingi elfu arubaini kila mmoja ili kufanikisha mauaji ya Cohen.  Aidha Kinoti amesisitiza kwamba Cohen aliuliwa chumbani kwake kabla kutupwa katika tenki hilo.