array(0) { } Radio Maisha | Makubaliano ya amani kati ya Kenya na Uganda yapongezwa

Makubaliano ya amani kati ya Kenya na Uganda yapongezwa

Makubaliano ya amani kati ya Kenya na Uganda yapongezwa

Na Esther Kirong',

Nairobi, Kenya,

Viongozi kwenye Kaunti ya Pokot Magharibi wameipongeza hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ya kuja pamoja na kutia saini makubaliano ya amani baina ya nchi hizo mbili, kwa lengo la kukomesha uvamizi miongoni mwa jamii za wafugaji zilizo mpakani hasa za  Pokot, Karamoja na Turkana.

Spika wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Catherine Mukenyang amekuwa wa kwanza kuipongeza hatua hiyo akitaja kuwa itatoa mwanga wa amani katika maeneo hayo yote.

Juhudi hizo za mpango wa Amani na Maendeleo ya Kudumu ya Mpakani zinakusudiwa kumaliza uhasama miongoni mwa jamii hizo tatu jirani na kuimarisha maendeleo katika eneo hilo kwa kukuza uhusiano na ushirikiano wa amani bila ghasia zozote.

Ikumbukwe mpango huo unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa utaongozwa na Kamati ya Mawaziri wa Kenya na Uganda na utatekelezwa katika eneo hilo ili kupunguza uhasama kutokana na matumizi ya rasilmali za pamoja kama vile maji na malisho kwa mifugo.