array(0) { } Radio Maisha | Kampuni ya SportPesa imepuuza madai kwamba inalenga kusitisha ufadhili

Kampuni ya SportPesa imepuuza madai kwamba inalenga kusitisha ufadhili

Kampuni ya SportPesa imepuuza madai kwamba inalenga kusitisha ufadhili

Kampuni ya SportPesa imepuuza madai kwamba inalenga kusitisha ufadhili kwa timu za humu nchini punde tu itakaporejelea shughuli zake za kawaida.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, SportPesa imesema itaendelea kutoa ufadhili kwa baadhi ya klabu lengo likiwa kuimarisha sekta ya michezo hasa kandanda.

Mkuu wa mawasiliano katika kampuni hiyo, Jean Kiarie amesema kwa sasa SportPesa inahakikisha imerejeshewa leseni yake na Bodi ya Kudhibiti Michezo ya Kamari ili kurejelea shughuli zake.

Kiarie amesema tayari kampuni hiyo imepewa idhini na Mamlaka ya Ukusanyaji Kodi, KRA baada ya kukamilisha kulipa kodi.

Ikumbukwe KRA ilizipokonya leseni kampuni ishirini na saba za bahati nasibu kwa kukwepa kulipa kodi ya mabilioni ya pesa.

SportPesa hutumia shilingi milioni 96 kila mwaka kutoa ufadhili kwa timu za Kenya. Shilingi milioni 55 hutumiwa kufadhili Klabu ya AFC Leopards huku shilingi milioni 65 zikifadhali Gor Mahia.

Mwezi Agosti mwaka huu, SportPesa ilitangaza kwamba ingesitisha ufadhili kwa timu za humu nchini huku KRA ikilaumiwa kwa kuzihujumu kampuni za michezo ya kamari.

KRA ilikuwa ikidai kampuni hiyo kodi ya shilingi bilioni 8.59 hali iliyoilazimu kuiagiza Kampuni ya Mawasiliano ya Safaricom kufunga nambari za kutuma na kutoa pesa, Paybill Numbers.