array(0) { } Radio Maisha | Ndindi Nyoro atetewa na wakaazi wa Kiharu

Ndindi Nyoro atetewa na wakaazi wa Kiharu

Ndindi Nyoro atetewa na wakaazi wa Kiharu

Wakazi wa Kiharu Kaunti ya Murang'a wanaendelea kumsuta Mbunge Maalumu, Maina Kamanda kwa kumshambulia mbunge wao, Ndindi Nyoro.

Kwa mujibu wa wakazi hao, Kamanda amekuwa akijitangaza kwamba ndiye mbunge wa eneo hilo kila uchao huku akidai kwamba Ndindi hafai kuwa kiongozi. Aidha, wakazi hao wamesema Kamanda amekuwa akimsihi Ndindi kujitenga na Kundi la Tangatanga linalomuunga mkono Naibu wa Rais, William Ruto na badala yake kuunga mkono Kundi la Kieleweke linalounga mkono Rais Uhuru Kenyatta ila juhudi zake zikaambulia patupu.

Vilevile, wamesema Kamanda amekuwa akimdhulumu Ndindi ilhali anapaswa kuwa kielelezo katika jamii hasa ikizingatiwa umri wake. Wamemwonya dhidi ya kuendesha siasa za kumpinga Naibu wa Rais katika Kaunti ya Murang'a na badala yake kuangazia siasa za Nairobi.

Wakati uo huo, wakazi hao wamesema mapatano kati ya Rais na Kinara wa ODM, Raila Odinga yanalenga kuhujumu demokrasia miongoni mwa Wakenya.

Aidha, wamemlaumu Kamishna wa kaunti hiyo na baadhi ya maafisa wa polisi kwa kumtetea Kamanda na hata kumpa ulinzi kila anapozuru kaunti hiyo. Wamesema polisi wanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuwahujumu viongozi wa Tangatanga.

Wamewaonya polisi dhidi ya kumtia mbaroni Ndindi.

Jumapili polisi walikita kambi nje ya Kampuni ya Royal Media kuanzia mwendo wa saa tatu unusu wakilenga kumkamata kufuatia mvutano kati yake na Kamanda katika Kanisa Katoliki la Gitui kwenye Eneo Bunge la Kiharu mvutano ambao ulitatiza ibada kanisani humo kwa muda.

Nyoro alikuwa amealikwa kwa mahojiano katika Runinga ya Inooro, mahojiano yaliyokamilika mwendo wa saa tatu unusu usiku japo alisalia kituoni humo kwa muda kisha kufanikiwa kutoweka bila kunaswa dakika chache kabla ya saa sita usiku.