array(0) { } Radio Maisha | Rais Kenyatta awaongoza viongozi wengine na Wakenya kumuomboleza Mugabe

Rais Kenyatta awaongoza viongozi wengine na Wakenya kumuomboleza Mugabe

Rais Kenyatta awaongoza viongozi wengine na Wakenya kumuomboleza Mugabe

Rais Uhuru Kenyatta amewaongoza viongozi wengine na Wakenya kutuma risala za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe ambaye amefariki dunia.

Rais Kenyatta amesema Wakenya wanaungana na taifa hilo wakati huu wa majonzi huku akiowambea jamaa, ndugu na watu wa Zimbabwe ambao kwa miaka mingi aliwatumikia kwa kujitolea na kwa bidii.

 ''Sina maneno ya kutosha kuelezea uzito wa kuaga dunia kwa kiongozi shupavu, shujaa na mzalendo wa Afrika ambaye alitekeleza jukumu muhimu katika kutetea maslahi ya bara la Afrika.

Bila shaka, tutamkumbuka Rais huyo wa zamani Robert Mugabe kuwa mtu jasiri ambaye kamwe hakuogopa kuelezea msimamo wake kuhusu jambo lolote hata kama wengi hawakumuunga mkono''

Kwa upande wake Naibu wa Rais, William Ruto amemtaja Mugabe kuwa kiongozi aliyejitolea kupigania uhuru na kuhakikisha amani inadumishwa Zimbabwe. Ruto amesema Mugabe atakumbukwa kuwa kiongozi aliyewapenda watu wake hivyo kuwafurusha watu wa mataifa mengine.

Wakati uo huo, Seneta wa Baringo Gideon Moi amemtaja Mugabe kuwa kiongozi jasiri aliyejitolea kuwahudumia wananchi wa Zimbwabwe.

Tayari Rais wa sasa wa Zimbwabwe, Emmerson Mnangagwa ametangaza kwamba bendera itapeperushwa nusu mlingoti nchini humo kumkumbuka kiongozi huyo aliyepigania uhuru kwa ujasiri.

Rais Mnangagwa amemtaja Mugabe kuwa kiongozi aliyefanya kila awezalo kusalia mamlakani hata kwa kuwafukuza watu walionekana kumbandua.

Hata hivyo, Mnangagwa amesema katika uongozi wa Mugabe, uchumi wa taifa hilo ulizorota mno hivyo wawekezaji kutoweka.