array(0) { } Radio Maisha | Gavana Alfred Mutua, amemlaumu Aden Duale kwa kulemaza juhudi za kutatua mzozo wa mgao kwa kaunti

Gavana Alfred Mutua, amemlaumu Aden Duale kwa kulemaza juhudi za kutatua mzozo wa mgao kwa kaunti

Gavana Alfred Mutua, amemlaumu Aden Duale kwa kulemaza juhudi za kutatua mzozo wa mgao kwa kaunti

Gavana wa Machakos, Daktari Alfred Mutua, ametoa wito kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justine Muturi kumwondoa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale katika Kamati ya Mariadhiano ya kutafuta suluhu kuhusu mzozo wa Ugavi wa Mapato kwa Serikali za Kaunti.

Gavana Mutua amesema kwamba Duale anaegemea upande mmoja katika mchakato huo akihofia kwamba huenda msimamo wake ukasambaratisha juhudi za kupatikana kwa mwafaka wa mzozo huo.

Mutua ambaye pia ni Kinara wa Chama cha Maendeleo Chap Chap, amesema mazungumzo baina ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu mvutano huo ni muhimu kwa wananchi mashinani ambao wamekosa huduma kutokana na kucheleweshwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti.

Mutua amesema kwamba mwafaka wa kamati hizo utasababisha kuimarika kwa ugatuzi na kukabili umaskini miongoni mwa Wakenya.

Amelalamikia mgao mdogo unaotengewa serikali za kaunti akisema hali hiyo imesababisha  kukwama kwa maendeleo hasa wakati huu ambapo wafanyakazi wengi na wasambazaji wa bidhaa na huduma wanalalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao.

Gavana huyo ametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati suala hilo,  akisema ni njia mojawapo ya kufanikisha ajenda zake nne za maendeleo.

Ikumbukwe kwamba umekuwapo mzozo baina ya mabunge haya mawili huku Seneti ikipendekeza kima cha shilingi bilioni 335 kwa kaunti tofauti na Bunge la Kitaifa ambalo linapendekeza na kuidhinisha mgao wa shilingi bilioni 316.