array(0) { } Radio Maisha | Seneta wa Nandi, Samson Cherargei sasa anadai kuwa alifasiriwa visivyo

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei sasa anadai kuwa alifasiriwa visivyo

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei sasa anadai kuwa alifasiriwa visivyo

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei sasa anadai kuwa alifasiriwa visivyo, katika kauli yake inayodaiwa kuwa ya uchochezi. Chergei ametoa kauli hiyo punde alipoachiliwa, baada ya kohojiwa na kurekodi taarifa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi, DIC, jijini Kisumu.

Cherargei ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Sheria katika Bunge la Seneti, ameachiliwa kwa bondi hiyo isiyorejeshwa iwapo atakosa kujiwasilisha mahakamani, akidokeza kuwa polisi wamesema bado wanaendeleza uchunguzi dhidi yake huku akidaiwa kukosa kushirikiana nao alipohitajika kufanya hivyo.

Hata hivyo Cherargei ameshikilia kwamba matamshi yake hayakuwa ya uchochezi huku akisema anasubiri uchunguzi ukamilike ili kubaini iwapo matamshi yake yangeibua uhasama miongoni mwa wananchi.

Seneta Cherargei aliwasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Central jijini Kisumu mwendo wa saa nane alasiri, baada ya kusafirishwa kutoka mjini Eldoret alikokamatwa akihusishwa na madai ya uchochezi.

Wakati wa tukio hilo, Gavana wa Nandi Stephen Sang', aliandamana na mawakili wa Cherargei ambaye anakabiliwa na madai ya kutoa matamshi yanayodaiwa kuwa yenye uchochezi wakati wa mazishi ya mwalimu mmoja katika eneo la Lelwak, O'lessos Kaunti ya Nandi.

Licha ya kupinga matamshi yaliyotolewa na seneta Cheragei, Gavana Sang' ameikashifu Idara ya Upelelezi DCI kwa madai ya kuingiza siasa utendakazi wake.

Sang' amesema DCI imeharakisha uchunguzi dhidi ya Cherargei kinyume na kawaida yake, hivyo kuibua maswali mengi kuhusu uhuru wa idara hiyo.

Haya yanajiri huku Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC ikikashifu vikali matamshi ya Cherargei.

Katibu wa NCIC, Hassan Mohammed amesema matamshi ya kiongozi huyo yanaweza kuibua uhasama miongoni mwa Wakenya hivyo kuwashauri wananchi kuyapuuza.

Hassan amesema, NCIC itaingilia kati kesi hiyo ili kuhakikisha Cherargei anawajibishwa kutokana na matamshi yake yanayofikirika kuwa yenye uchochezi.

Ikumbukwe jana Idara ya Upelelezi, DCI ndiyo iliyomwagiza Cherargei kwenda kurekodi taarifa baada ya kanda ya video kusambaa mitandaoni, kabla ya NCIC kujitokeza leo kufuatia kisa hicho.