array(0) { } Radio Maisha | Kipchumba Murkomen atofautiana na Naibu Gavana Wesley Rotich

Kipchumba Murkomen atofautiana na Naibu Gavana Wesley Rotich

Kipchumba Murkomen atofautiana na Naibu Gavana Wesley Rotich

Seneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti ametofautiana vikali na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Wesley Rotich kuhusiana na mgao wa fedha wa kaunti.

Rotich amelalamikia mgao mdogo wa fedha zilizotengewa kaunti hiyo akidai kuwa hauwezi kutosheleza mahitaji akimtaka Senata Murkomen kusaidia kupasisha mswada uliopo katika Bunge la Sneti kuhusu mgao wa fedha ili kuhakikisha kuwa kaunti hiyo inaongezewa fedha hadi angalau shilingi bilioni 5 ikilinganishwa na bilioni 3.7 ya sasa.


Ni madai ambayo yamekashifiwa vikali na Seneta Murkomen akidai kuwa mgao wa fedha hutolewa kulingana na idadi ya wakaazi wa kaunti.

Kwa mujibu wa Murkomen Serikali ya Kaunti ya Elgeiyo Marakwet imekosa kuwajibikia fedha zake ipasavyo.

Murkomen anaitaka serikali hiyo kuchunguza orodha ya wafanyikazi na kuwatambua wafanyikazi hewa ambao wamesababishia kaunti hiyo kutumia fedha nyingi kugharamia mishahara.

Wawili hawa walikuwa wakizungumza katika hafla ya kuwataza  Makasisi wa Kanisa la AIC Mjini Iten

Ikumbukwe Serikali ya Kaunti ya Elgeiyo Marakwet kufikia sasa bado haijawalipa wafanyikazi wake mshahara wa mwezi wa Julai kwa madai kuwa kaunti hiyo haina fedha za kutosha huku wauguzi wakitishia kugoma iwapio kufikia leo hawatakuwa wamelipwa.

Hata hivyo, saa chache baada ya Seneta wa Kaunti ya Elgeiyo Marakwet Kipchumba Murkomen kuukashifu uongozi wa kaunti hiyo, Gavana Alex Tolgos amejitokeza na kudai kuwa seneta huyo ana njama fiche kuhusiana na uongozi wake.


Kupitia taarifa kwa yyombo vya habari , Gavana Tolgos amemtuhumu Murkomen kwa madai ya kujiunga na wawakilishi wadi kwa lengo la kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni na kumwondoa mamlakani.


Kuhusu madai ya Murkomen kuwa kaunti hiyo ina idadi kubwa ya wafanyikazi hewa Tolgos amemtaka seneta huyo kuzuru ofisi za kaunti hiyo kuwatambua.
Aidha Tolgos amemtuhumu Seneta Murkomen kwa kutumia bunge la kaunti hiyo kuhujumu utendakazi wake na kumharibia jina.


Seneta Murkomen anatarajiwa kutoa taarifa kuhusu   madai haya leo mchana.