array(0) { } Radio Maisha | Wakazi wa Kangemi wasusia kushiriki Sensa
Wakazi wa Kangemi wasusia kushiriki Sensa

 

Usalama ungali umeimarishwa mtaani Kangemi, baada ya wakazi kuzua vurugu mapema leo, wakilalamikia kutengwa katika shughuli ya kushiriki mafunzo ya kuendesha sensa.

Wakazi hao ambao walikivamia Kituo cha Kihumbini, wamemlaumu chifu wa eneo hilo, ambaye wanadai alihongwa na baadhi ya watu wa sehemu nyingine jijini Nairobi ili kuwaweka katika orodha ya wale ambao wameteuliwa kuendesha shughuli hiyo ya sensa. Wameapa kuwa iwapo malalamiko yao hayatashughulikiwa hatatakubali kuhesabiwa.

Aidha, wanataka mafunzo kwa maafisa ambao tayari wameteuliwa yasitishwe, hadi wenyeji watakapojumuishwa.

Awali, Mbunge wa Westlands - Tim Wanyonyi alisema orodha ya wanaofunzwa itakaguliwa ili kubaini iwapo madai ya wakazi ni ya kweli au la.

Hiki si kisa cha kwanza kushuhudiwa kuhusu utaratibu unaotumika kuwafunza maafisa hao. Visa sawa na hicho vimeshuhudiwa kwenye kaunti mbalimbali zikiwamo, Nyamira, Kiambu na Bungoma.

Haya yanajiri siku tano tu baada ya wakazi watano wa Kaunti ya Homa Bay kuwasilsiha kesi mahakamani kulitaka Baraza la Kitaifa la Uhesabu wa Watu (KNBS) kuzuiwa kufanya ya sensa katika kaunti hiyo.

Watano hao - Michael Otieno, Evance Oloo, John Okambo, Antony Gaya na Daniel Otieno Onyango wanaishtumu KNBS kwa kukiuka utaratibu wa kuwachagua maafisa wa akuendesha shughuli hiyo.

Mwaka huu, jumla ya maafisa elfu mia moja sabini na nne mia saba, watateuliwa kuendesha shughuli hiyo itakayofanyika tarehe 24, 25 na 26 mwezi huu.