array(0) { } Radio Maisha | Serikali yaombwa kuimarisha usalama wakati wa Sensa.

Serikali yaombwa kuimarisha usalama wakati wa Sensa.

Serikali yaombwa kuimarisha usalama wakati wa Sensa.

Serikali  imeombwa kuwahakikishia wananchi usalama wa kutosha wakati wa shughuli ya sensa hasa ikizingatiwa shughuli hiyo itafanyika usiku. Mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu, amesema huenda wahalifu wakachukua fursa hiyo kutekeleza visa vya uhalifu miongoni mwa Wakenya.

Kauli yake inajiri huku serikali ikisema imeweka mikakati kuhakikisha sensa inaendeshwa bila kushuhudiwa utovu wa usalama. Waziri wa Leba, Ukur Yattani aidha amesema mikakati imewekwa ili kuhakikisha kila Mkenya anashiriki shughuli hiyo.

Waziri Yattani amesema wafanyakazi wa kutosha wameajiriwa ili kuendesha shughuli hiyo muhimu.

Yatani ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Fedha aidha amesema kwamba vifaa vyote vya kielektroniki vimethibitishwa kuwa sawa kwa utumizi wakati wa sensa. Amepuuza madai kwamba simu na tarakilishi zilizonunuliwa zinaweza kupoteza data za Wakenya.

Amesema shughuli ya sensa iliyofanyiwa majaribio mwaka wa 2017 ilihakikisha kwamba vifaa vyote viko salama kwa shughuli hiyo.

Haya yanajiri huku Wizara ya Elimu ikitoa tangazo la kuongezwa likizo ya muhula wa pili kwa wiki moja zaidi ili kuruhusu wanafunzi kushiriki shughuli ya sensa. Katibu katika wizara hiyo, Belio Kipsang, amesema shule sasa zitafunguliwa tarehe mbili mwezi septemba badala ya tarehe 26 mwezi huu.