array(0) { } Radio Maisha | Jopo la Upatanishi BBI lakutana na viongozi wa kidini

Jopo la Upatanishi BBI lakutana na viongozi wa kidini

Jopo la Upatanishi BBI lakutana na viongozi wa kidini

Jopo la Upatanishi BBI linaendelea kupokea maoni ya viongozi mbalimbali wa Kidini na wanasiasa kuhusu marekebisho ya katiba kwa lengo la kuboresha uongozi wa taifa hili kwa manufaa ya Wakenya katika Ukumbi wa KICC.

Aliyekuwa mwaniaji wa ugavana kwenye Kaunti ya Busia, Paul Otuoma ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Usimamizi wa Taasisi Binafsi Nchini, amesema sheria inafaa kubuniwa ili kuweka wazi mahitaji ya kumshinikiza kiongozi kujiuzulu anapohusishwa na ufisadi.

Otuoma ambaye pia alikuwa Mbunge wa Funyula, aidha amesema sheria ya kuvidhibiti vyama vya kisiasa inafaa kubuniwa ili kukabili udikteta katika vyama hivyo, hali ambayo imechangia kuwapo kwa uongozi wa binafsi.

Vilevile, viongozi wa Dini ya Kiislamu wakiwajumuisha wanasiasa akiwamo Suleiman Shahbal aliyewania ugavana wa Mombasa katika uchaguzi mkuu uliopita, wamependekeza serikali kubuni Wizara ya Masuala ya Wakenya wanaoishi mataifa ya Kigeni kwa jina Diaspora ili kuangazia maslahi yao.

Wamesema Wakenya hao wameshiriki pakubwa katika ukuaji wa kiuchumi hivyo kutakiwa kujumishwa serikalini ikizingatiwa kwamba mchango wao ni mkubwa ukilinganishwa na ule wa Wizara ya Utalii.

Kuhusu suala la chama kinachopata ushindi wa urais kuwa na majukumu ya kuwateua mawaziri, makatibu wa wizara, wakuu wa taasisi za serikali na mabalozi bila mchango wa walioshindwa uchaguzini, Shahbal amependekeza kubuniwa kwa sheria itakayovihusisha vyama vyote vya kisiasa katika uteuzi wa nafasi hizo ili kuepuka mivutano ya kisiasa.

Kikao hicho kitaendelea hadi jioni ambap leo ni siku ya mwisho kwa jopo la BBI kupokea maoni ya Wakenya, ambapo makundi mengine ambayo yangetaka kuwasilisha maoni yao yana hadi saa kumi na moja ya leo jioni kufanya hivyo.

Jana, viongozi wa kike wa Kundi la Embrace pamoja na vijana waliwasilisha maoni yao mbele ya jopo hilo wakipendekeza kuongezwa kwa nyadhifa za uongozi wa akina mama na kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu.