array(0) { } Radio Maisha | Wito kwa Wizara ya Ardhi kutatua mzozo wa ardhi Naivasha

Wito kwa Wizara ya Ardhi kutatua mzozo wa ardhi Naivasha

Wito kwa Wizara ya Ardhi kutatua mzozo wa ardhi Naivasha

Wizara ya Ardhi imetakiwa kusuluhisha mzozo wa umiliki wa kipande cha ardhi kinachozozaniwa katika eneo la Ndabibi mjini Naivasha katika Kaunti ya Nakuru hasa baada ya vijana kuvamia mashamba na kuvunja nyumba kadhaa kufuatia utata wa ardhi hiyo inayoaminika kuwa yenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Wakazi wa eneo hilo aidha wamelilaumu Shirika la Maendeleo ya Kilimo, ADC wakisema limechangia pakubwa katika kushuhudiwa kwa mizozo ya mara kwa mara.

Wakazi hao wanaojumuisha, wafanyakazi wa zamani wa taasisi mbalimbali za serikali wameapa kuendelea kuishi katika kipande hicho cha ardhi, wakisema wameishi hapo kwa zaidi ya miaka kumi.

Kwa mujibu wa Jonathan Nkoiboni ambaye ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo, mzozo wa kutaka kufurushwa kwa wakazi wanaoishi eneo hilo sasa umekuwa ukitekelezwa kila mwaka na hasa ukiilenga jamii moja miongoni mwa zile zinazoishi katika ardhi hiyo.

Nkoiboni aidha amesema jamii hiyo haitakubali kuhangaishwa huku ikimwomba Rais Uhuru Kenyatta na wabunge wa eneo hilo kuwasaidia kupata haki ya kumiliki ardhi yao.


Kauli yake imesisitizwa na mmoja wa walioathirika - Silvester Kamamia ambaye amekiri kupata hasara kubwa baada ya nyumba yake kuvunjwa.

Kamamia amesema wengi wa walioathirika na ubomoaji huo ni wale waliokuwa wafanyakazi wa taasisi za serikali ambao waliwekeza katika kipande hicho cha ardhi.

Hata hivyo, mmoja wa maafisa wa ADC katika eneo hilo amekana madai yaliyoibuliwa na wakazi hao, akisema Meneja Mkuu wa ADC jijini Nairobi atatoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo.