array(0) { } Radio Maisha | Joho kurejea nchini baada ya kukashifiwa mitandaoni

Joho kurejea nchini baada ya kukashifiwa mitandaoni

Joho kurejea nchini baada ya kukashifiwa mitandaoni

Gavana wa Mombasa Hassan Joho anatarajiwa kurejea nchini kesho kutoka Marekani ambako amekuwa kwa ziara ya binafsi tangu tarehe 16 mwezi Julai, ziara ambayo imeibua hisia mseto kutoka kwa wananchi.

Joho anakashifiwa kwa kwenda kuvinjari Marekani, ikizingatiwa picha na video alizochapisha katika mtandao wake wa Instagram akiwa na mwanamtindo na mwanamziki wa Marekani, Paris Hilton wakiwa wameshikana viunoni.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii - Facebook na Twitter wameendelea kumkashifu gavana huyo kwa kujistarehesha ughaibuni wakati Kaunti ya Mombasa ikiendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali ukiwamo utovu wa usalama.

"Kiongozi wetu yu Marekani akipiga picha na kutundika mitandaoni wakati kundi la Wakali Kwanza linatuhangaisha', Mwalimu Bosibori alichangia mjadala huo katika ukurasa wake wa Twitter.

Mwanaharusi - Jumma katika Facebook, anasema mpigakura ndiye wa kulaumiwa kwa kutowachagua viongozi waadilifu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwenye Kaunti ya Mombasa Richard Chacha amemtetea Joho akisema kwamba shughuli zote za kaunti zinaendelea bila tashwishwi licha ya gavana huyo kutokuwepo.

Aidha, Chacha amesema kwamba tangu kuondoka kwa Joho tarehe mapema mwezi Julai mwaka huu, kiongozi huyo amekuwa akihudhuria mikutano kadhaa na washikadau mbalimbali ambayo anasema ni ya manufaa kwa wakazi wa Mombasa.