array(0) { } Radio Maisha | Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitui ajiuzulu

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitui ajiuzulu

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitui ajiuzulu

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kaunti ya Kitui John Kisangau amejiuzulu. Kisangu anadai  kwamba serikali ya kaunti hiyo imekuwa ikimshurutisha katika kutekeleza maamuzi katika nafasi hiyo.

Kisangau, ambaye ni Mwakilishi wa Wadi ya Yatta-Kwavonza na ambaye alichaguliwa kupitia tiketi ya chama cha NARC Kenya kinachoongozwa na Gavana Charity Ngilu, amesema hangeweza kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo .

Akihutubia bungeni, Kisangau alikiri kuwa amepitia wakati mgumu katika kutetea serikali na utawala wa gavana Ngilu ambapo wakati mwingine maamuzi yanayofanywa katika serikali hiyo hayaendani na matakwa ya wananchi.

Kwa mujibu wa Kisangau, licha ya bunge la kaunti hiyo kupitisha na hata kuidhinisha  miradi katika kaunti hiyo, serikali ya kaunti ya Kitui imekuwa ikikosa kuitekeleza.

Aidha amekiri kuwa mara si moja amekuwa akimueleza gavana Ngilu kuhusu miradi hiyo ila hoja zake zimekuwa zikipuuzwa.

Aidha amesema uongozi wa serikali hiyo umekuwa ukiingilia utendakazi wa bunge na hivyo kukosekana kuwapo kwa uwazi na haki kwa wananchi.

Amesema kamati ya bunge la kaunti hiyo ya uteuzi imekuwa ikihitilafiana na namna ya kuwapiga msasa mawaziri na maafisa wengine katika serikali hiyo.