array(0) { } Radio Maisha | Mvutano waendelea baina ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti

Mvutano waendelea baina ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti

Mvutano waendelea baina ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti

Serikali za Kaunti zitalazimika kuendelea kusubiri hata zaidi kabla ya kupata mgao wa fedha kutoka kwa Serikali Kuu kufuatia mvutano unaoendelea baina ya Bunge la Kitaifa na Seneti.

Kwa mara nyingine Seneti imefutilia mbali mswada wa Bunge la Kitaifa unaopendekeza serikali za kaunti zitengewe jumla ya shilingi bilioni mia tatu kumi na sita nukta tano katika mgao wa bajeti mwaka huu, na badala yake kuufanyia marekebisho na kuongeza kiwango hicho cha fedha hadi shilingi bilioni mia tatu thelathini na tano nukta sita. Aidha maseneta wameondoa shilingi bilioni 6.2 zilizokuwa zimetengewa mpango wa ununuzi wa vifaa vya matibabu kwa kaunti zote arubaini na saba.

Naibu wa Spika wa seneti Kithure Kindiki amelikosoa Bunge la Kitaifa kwa kuendelea kuibua mvutano huku huduma katika serikali za kaunti zikiendelea kulemazwa. Amesema seneti itaendelea kutekeleza wajibu wake kikatiba kwa kuulinda ugatuzi.

Kauli hiyo imesisitizwa na Kiongozi wa Wachache katika Seneti Moses Wetangula akisema sharti mapendekeo ya Mamlaka ya Ugavi wa Mapato CRA yazingatiwe.

Ikumbukwe Alhamisi wiki Mahakama ya Juu iliahiisha keshi iliyokuwa imewasilishwa na Baraza la Magavana dhidi ya Bunge la Kitaifa kuhusu mvutano huo, baada ya kamati maalum ya majadiliano kukosa kuafikiana kuhusu kiwango cah fedha kinachostahili kutengewa serikali za kaunti.

Jaji Mkuu David Maraga aliwapa maspika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti siku kumi na nne kujaliana kuhusu mvutano huo, kabla ya kesi hiyo kutajwa tena tarehe 15 mwezi huu. Tayari wafanyakazi wa serikali za kaunti wametoa makataa hadi wiki ijayo walipwe mishahara yao ambayo imecheleweshwa kufuatia mvutano huo, la si hivyo wagome.