array(0) { } Radio Maisha | Barchok kuapishwa rasmi Alhamisi kuwa Gavana wa Bomet

Barchok kuapishwa rasmi Alhamisi kuwa Gavana wa Bomet

Barchok kuapishwa rasmi Alhamisi kuwa Gavana wa Bomet

Daktari Hillary Barchok Naibu Gavana wa Bomet, atachukua rasmi wadhfa wa ugavana leo hii atakapoapishwa. Shughuli hiyo itakayohudhuriwa na viongozi kadhaa itafanyika katika uwanja wa Green Stadium Mjini Bomet huku Naibu wa Rais William Ruto akiwa mgeni wa heshima. Wengine watakaohudhuria hafla hiyo kwa mujibu wa ratiba ya hafla ya leo ni Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliff Oparanya na baadhi ya mawaziri.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Kericho George Dullu ndiye atakayeiongoza shughuli yenyewe.

Wadhifa huo ulisalia wazi kufuatia kifo cha Joyce Laboso , aliyefariki dunia tarehe 29 Julai kufuatia saratani ya yai la kizazi. Laboso alizikwa tarehe 3, Agosti nyumbani kwake eneo la Koru Kaunti ya Kisumu.

Hayo yanajiri, huku shinikizo likizidi kutolewa na Barchok kuhakikisha kwamba anamchagua mwanamke kuchukua nafasi ya Naibu gavana. Ikumbukwe wakati wa mazishi ya Laboso, Barchok aliahidi kuitekeleza miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na Marehemu Laboso.

Kwa mujibu wa sehemu ya 182 ya katiba , iwapo wadhifa wa ugavana utasalia wazi kutokana na sababu mbalimbali kwa mfano anapoaga dunia akiwa ofisini, ajiuzulu kwa kumwarifu spika wa bunge la kaunti kupitia maandishi au ang'atuliwe ofisini, basi nafasi hiyo itachukuliwa na naibu wake.

Ikumbukwe Barchok atakuwa gavana wa tatu wa Bomet baada ya Isaac Ruto aliyehudumu wakati wa muhula wa kwanza tangu mwaka 2013 na kushindwa na Laboso wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.