array(0) { } Radio Maisha | Je, unafahamu ni kwa nini mama anastahili kumyonyesha mwanawe kwa miezi 6

Je, unafahamu ni kwa nini mama anastahili kumyonyesha mwanawe kwa miezi 6

Je, unafahamu ni kwa nini mama anastahili kumyonyesha mwanawe kwa miezi 6

Leo ikiwa ni siku ya kuadhimisho unyonyeshaji Duniani, akina mama wamehimizwa kuzingatia usafi wakati wanawanyonyesha wanao. Je, unafahamu ni kwa nini mama anastahili kumyonyesha mwanawe kwa miezi sita mfululizo bula kumpa chakula chochote kingine

Dang'a yaani colostrum ambayo ni maziwa ya kwanza baada ya mama kujifungua ni muhimu kwa mtoto kwani humpa kinga dhidi ya magonjwa aina aina. Maziwa haya pia yana virutubishi anavyohitaji mtoto, yana protini na madini ya cabohydrates kwa kiwango kinachohitajika. Asilimia themanini na nane ya maziwa ni maji kwa hivyo mama hana haja ya kumpa mtoto maji. Watoto wanaopewa vyakula vingine wamo katika hatari ya kupata magonjwa ya kisukari, leukemia na pumu yaani asthma.

Vilevile akina mama wanashauriwa kuzingatia usafi wanaponyonyesha. Mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Machakos Level 5, Charity Lemurua anaeleza ni muhimu kwamama kuosha mikono baada ya kumbadilisha mtoto nepi na kutoka msalani. 

Lemurua anawashauri akina mama kuzingatia usafi wa titi ili wanaponyonyesha, vilevile akawaonya akina mama dhidi ya kupaka titi mate kabla ya kunyonyesha, kwani mate hubeba virusi vingi.

Vilevile kuna baadhi ya wanawake ambao hawana maziwa ya kutosha baada ya kutumia tembe ama sindano za upangaji uzazi zinazochangia mabadiliko ya homoni mwilini. Wanawake wengine hukosa maziwa kwa sababu za kimaumbile, pengine mishipa ya maziwa. Hata hivyo hali hii inaweza kuangaziwa kupitia ushauri wa daktari. Pia, mama anaweza tumia vifaa vya kuvuta maziwa yaani pumping.

Uwezekano wa mama anayeugua saratani ya matiti kumnyonyesha mwanawe unategemea na jinsi ugonjwa huo umeenea na matibabu anayopokea. Kwa mujibu wa wataalam upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye matiti unaweza kupunguza maziwa ya mama endapo mishipa iliathirika. Hata hivyo, mama anaweza kuendelea kumnyonyesha mwanawe baada ya kupona. Matibabu aina ya chemotherapy na radiotherapy hutumia kemikali ambazo zinaweza kumdhuru mtoto.

Mama aliye na virusi vya HIV anaweza kumnyonyesha mwanawe bila kumwambukiza akimeza dawa za kupunguza makali yake, yaani ARV's wakati wa ujauzito na kuendelea hata wakati wa kumnyonyesha. Vilevile mtoto anapozaliwa bila virusi hivyo hupewa dawa ya kuzuia maambukizi iitwayo nevirapine, kisha kupimwa tena baada ya wiki sita na kuendelea kupimwa hadi atakapofikisha miezi kumi na minane.