array(0) { } Radio Maisha | Wakenya wahofia usalama wakati wa shughuli ya sensa

Wakenya wahofia usalama wakati wa shughuli ya sensa

Wakenya wahofia usalama wakati wa shughuli ya sensa

Zikiwa zimesalia wiki tatu tu kabla ya kuanza kwa shughuli ya Kitaifa ya Sensa, serikali imetenga kima cha shilingi bilioni 18.5 kufanikisha shughuli hiyo huku hakikisho likitolewa kwamba shughuli yenyewe itafanyika vyema.

Wakenya wengi wanahofia usalama wao wakati wa shughuli ya sensa wakitaka kujua ni vipi watakavyotambua watakaobisha nyumba zao iwapo ni maafisa wa sensa au wahalifu. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Takwimu, KNBS maafisa hao watakuwa na stakabadhi za mamlaka hiyo za kuwatambulisha, watavaa jaketi zilizo na maandishi ya KNBS na muhimu kabisa kuandamana na kiongozi wa kijiji, nyumba kumi au mkazi anayejulikana na wanakijiji. Baada ya kuhesabiwa maafisa hao wataweka maandishi nje ya mlango ili kuzuia hesabu kufanywa kwa mara ya pili.

Vilevile ukiwa safarini au katika hoteli muradi uko ndani ya mpaka wa Kenya utahesabiwa, tofauti ni fomu itakayotumiwa haitafanana na itakayotumiwa na waliohesabiwa wakiwa nyumbani. KNBS Imetoa fomu 5- moja kuu itakayotumika katika makazi na nne fupi zitakazotumika kwa watakaokuwa safarini, hotelini, shuleni na gerezani.

Je, wajua umuhimu wa sensa Umuhimu wake ni kurahisisha shughuli za uundaji wa bajeti ya nchi, ugavi wa rasilmali, kuirahisishia serikali mchakato wa utoaji wa vitambulisho kwa raia wake, sensa hutumika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa katika kila eneo nchini, kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, mapato yao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi.

Sensa vilevile hutumika kudhibiti idadi ya wananchi, mfano baada ya sensa ikibainika kuwa idadi ya watu imeongezeka kwa kasi mno hadi kuathiri uchumi wa taifa basi serikali hutoa mafunzo kuhusu ngono, upangaji uzazi, kuwapunguzia kodi wanandoa wanaoamua kupunguza idadai ya watoto wanaotarajia na kuwazuia raia wa kigeni wanaopanga kuhamia nchini kabisa.

Aidha, baada ya sensa ikibainika kuwa idadai ya watu ni ndogo hadi kuathiri uchumi wa taifa basi serikali huwahamasisha wanandoa kuongeza idadi ya watoto, kutoa marupurupu ya kufunga ndoa na kuruhusu raia wa kigeni kuingia nchini na kuishi kwa urahisi.

Mkurugenzi Mkuu wa KNBS, Zachary Mwangi anasema kuwa iwapo usiku wa tarehe 24 mwezi huu utakuwa nchini Kenya, basi bila shaka utahesabiwa katika shughuli ya sensa uwe Mkenya au raia wa kigeni.  Iwapo hutakuwa nyumbani tarehe hiyo, utahesabiwa tarehe 31 mwezi huu.

Vilevile mwaka huu, shughuli hiyo itafanywa kielektroniki, na mashine hizo 164700 zilitengenezwa humu nchini na wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Moi na JKUAT huku mashine moja ikiuzwa kwa shilingi 15,000.

Hii itakuwa shughuli ya 7 ya sensa kufanyika nchini. Ya kwanza ilifanyika 1948, kisha miaka kumi na minne baadaye yaani mwaka wa 1962, kisha baada ya miaka saba yaani mwaka wa 1969, baadaye ndipo taifa lilianza kufanya hesabu hiyo baada ya kila miaka kumi ikianza na mwaka 1979, 1989, 1999, 2009, na mwaka huu 2019, ambapo itafanyika kuanzia tarehe 24-31 Agosti.