array(0) { } Radio Maisha | Ahudhuria vikao vya bunge na akiwa na mtoto.

Ahudhuria vikao vya bunge na akiwa na mtoto.

Ahudhuria vikao vya bunge na akiwa na mtoto.

Katika hali inayofasiriwa kuwa ya kushinikiza kuanzishwa kwa eneo la wabunge wa kike kunyonyeshea, na wanao kuchezea bungeni, vilevile kuendana na wiki ya uhamasiho kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji duniani, Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kwale Zulekha Hassan amehudhuria vikao vya bunge akiwa na mtoto mchanga. Hatua hiyo imewaghadhabisha baaadhi ya wabunge ambao wamemshtumu mwakilishi huyo wakisema amekiuka sheria za bunge.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Adan Duale, amesema watoto wachanga kwa mujibu wa sheria za bunge hawaruhusiwi kuingia vikaoni.

Ilimlazimu Spika wa muda, Chris Muchelule kumfurusha mbunge huyo na kusema angeruhusiwa kuhudhuria vikao bila mtoto.

Muchelule amesema bunge limetoa nafasi na muda unaofaa kwa akina mama kuwahudumia wanao nje ya ukumbi wa bunge. Amewaonya wabunge ambao watakiuka sheria za bunge kwamba wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, wabunge wanawake wameandamana na Zulekha na kuondoka vikaoni huku wakisema hakuna sehemu iliyotengwa kwa ajili ya watoto wachanga licha ya bunge kuidhinisha sheria. Zulekha kwa upande wake amejitetea na kusema alikuwa na dharura hali iliyomlazimu kuhudhuria vikao akiwa na mwanawe mchanga.

Kulingana na sheria za Bunge la Kitaifa Standing Orders hakuna yeyote anayestahili kuingia katika ukumbi wa bunge bila idhini ya Spika wa Bunge.

Si kawaida kwa wabunge nchini kuingia katika ukumbi huo wakiwa na watoto wa changa mara ya kwanza kisa kama hicho kutokea ilikuwa mwaka 2013 wakati Seneta maalum, Sarah Korere ambaye sasa ni Mbunge wa Laikipia Kaskazini kumnyonyesha mwanawe mchanga akiwa anahuduria vikao. Kisa hicho kilibua hisia kali hasa miongoni mwa viongozi wenzake waliomshtumu vikali.

Hata hivyo katika baadhi ya mataifa si ajabu kwa viongozi kuhudhuria vikao wakiwa na wanao wachanga. Mwaka 2016 Bunge la Australia lilipitisha sheria kuwaruhusu kina mama walio na wanao wachanga kuingia nao vikaoni na hata kuwanyonyesha.