array(0) { } Radio Maisha | Wakali kwanza wavamia wakazi Bamburi.

Wakali kwanza wavamia wakazi Bamburi.

Wakali kwanza wavamia wakazi Bamburi.

Watu wanane wanaendelea kutibiwa majeraha mabaya waliopata baada ya kuvamiwa na kundi la vijana zaidi ya kumi eneo la Lake View, Bamburi, eneo Bunge la Kisauni.

Vijana hao wanaaminika kuwa wanachama wa kundi la Wakali Kwanza walikuwa wamevalia jaketi maalum na walianza kuwavamia kiholela wapita njia kuanzia Shule ya Msingi ya Bashir kuelekea kijiji cha Soweto.

Walioshuhudia tukio hilo wameiambia Radio Maisha kwamba vijana hao waliwakatakata kwa panga yeyote waliyempata njiani kabla ya polisi kufahamishwa na kuwasili eneo hilo kudhibiti hali.

Milio ya risasi ilisikika baadaye katika maeneo ya Bamburi Mwisho, Mtopanga na Kadzandani huku polisi wakidokeza kwamba waathiriwa walikuwa na majeraha ya kukatwa kichwani, tumboni, shingoni, mgongoni, mikono na miguu. Wasamaria wema waliwakimbiza katika zahanati ya Yeshua Medicare walikopewa Huduma ya Kwanza kabla ya kukimbizwa katika Hospitali ya Coast General.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi kwenye Kaunti hiyo Johnstone Ipara amewaonya wanaowasadia wahalifu hao kujificha kwamba watakabiliwa kwa mjibu wa sheria.

Kamishna wa Kaunti hiyo Evans Achoki amesema kwamba walifanikiwa kudhibiti hali kwa wakati huku akitarajiwa kutoa ripoti kamili kuhusu tukio hilo baadaye leo hii.

Mkuu wa wauguzi katika Hospitali hiyo amesema kwamba wanaume watatu wamelazwa hospitalini humo wakiwa na majeraha mabaya kwenye kichwa na kwamba hali yao inaendelea kuimarika.