array(0) { } Radio Maisha | Viongozi wamemiminia sifa marehemu Joe Kadenge kwenye misa yake

Viongozi wamemiminia sifa marehemu Joe Kadenge kwenye misa yake

Viongozi wamemiminia sifa marehemu Joe Kadenge kwenye misa yake

Jumbe za sifa zimeenea katika Ibada ya wafu ya aliyekuwa mwanasoka tajika Joe Kadenge katika kanisa la Friends International  hapa jijini Nairobi.

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amemtaja Kadenge kuwa mtu mungwana aliyejawa na utu huku akisema alijitolea katika kufanikisha historia ya mchezo wa soka nchini. Odinga amesema Vijana wanapaswa kuiga mfano wa Kadenge, kwani alikuwa muadilifu na hekima ya hali ya juu.

Amesema kitabu cha Kadenge kinasimulia namna alivyokua kwenye ulingo wa soka.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula ameeleza kusikitishwa na jinsi ambavyo viongozi nchini wamekuwa na hulka ya kusifia watu pindi wanapoaga dunia badala ya kufanya hivyo wakati wangali hai.

Wetangula amerudia pendekezo ambalo limekuwapo kuwa Bunge linapaswa kuja na mbinu za kuhakikisha maslahi ya wanasoka yanaafikiwa ili kuinua viwango vya michezo nchini.

Kauli hiyo imetiliwa mkazo na Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi ambaye amelihimiza bunge kubuni sheria itakayoboresha maisha ya wachezaji si tu wa soka bali michezo yote ambayo taifa hili inashiriki.

Mwili wa Kadenge utasafirishwa kesho hadi maeneo ya Vihiga ambako anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi.