array(0) { } Radio Maisha | Kaunti zatumiwa kiwango kidogo cha fedha kuwahudumia wananchi

Kaunti zatumiwa kiwango kidogo cha fedha kuwahudumia wananchi

Kaunti zatumiwa kiwango kidogo cha fedha kuwahudumia wananchi

Kaunti nyingi nchini zimetumia asilimia chini ya 50 ya bajeti katika miezi tisa ya mwaka wa kifedha 2018/ 2019. Hali hii ina maana kwamba Wakenya hawajawa wakihudumiwa licha ya kulipa kodi kwa wakati.

Kwa mujibu wa ripoti ya bajeti ya serikali za kaunti, kaunti zilitumia asilimia 48.4 ya bajeti kila mwaka.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Kaunti ya Narok pekee ndiyo iliyotumia bajeti yake vizuri kwa asilimia 60.1 ya fedha zilizotengewa serikali hiyo.

Miongoni mwa kaunti kumi bora ambazo zilitumia bajeti vizuri ni Kitui, Garissa, Taita Taveta, Murang’a, Mandera, Nairobi, Nandi, Nyamira na Kakamega.

Narok ilitumia asilimia 66.9 ya bajeti, Kitui asilimia 59.6, Garissa 57.6, Taita Taveta 56.9, Murang'a 56.0, Mandera 55.7, Nairobi 55.3, Nandi 55.0, Nyamira 54.7 sawa na Kakamega.

Aidha, kaunti kumi zilizofanya vibaya sana kwa kutotumia bajeti yake kwa miradi ya maendeleo kuwanufaisha wakazi ni pamoja na Wajir kwa asilimia 32.9, Nakuru 35.6, Kilifi 36.1, Lamu 37.1, Tana River 37.9, Siaya na Nyandarua asilimia 39.9, Kajiado asilimia 41.2, Baringo 41.7, Samburu 42.7 na Turkana asilimia 43.9.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Kakamega ilitumia shilingi milioni tatu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikifuatwa na Mandera na Nairobi kwa shilingi milioni 2.8 na milioni 2.3 mtawalia.

Gavana Wycliffe Oparanya alitumia shilingi milioni 545.7 katika ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Bukhungu, shilingi milioni 341.2 katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kakamega, milioni 260.8 kukamilisha ujenzi wa barabara kilomita kumi katika kila wadi huku shilingi milioni 102.5 zikitumika kufanikisha mipango ya mji wa Kakamega.

Aidha, Gavana Mike Sonko wa Nairobi alitumia shilingi milioni 300 katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo. Shilingi milioni 119 kukarabati barabara kadhaa mjini na shilingi milioni 105.5 kujengea Barabara ya Jodongo. Aidha, Sonko alitumia shilingi milioni 167 kujenga barabara kadhaa katika Mtaa wa Utawala.

Kaunti ya Mandera, ilitumia shilingi milioni 400 katika ujenzi wa barabara, shilingi milioni 119 kufanikisha ujenzi wa majumba ya wakimbizi, milioni 112 kukamilisha ujenzi wa majumba ya kulala katika kaunti hiyo na shilingi milioni 100 kukamilisha ujenzi wa afisi za kaunti.

Wakati uo huo, Kaunti ya Wajir ilitumia shilingi milioni 464 kukarabati barabara, kufyeka msitu barabarani vilevile kutia lami. Aidha, shilingi milioni 492 zilitumika katika uchimbaji mabwawa.

Gavana Lee Kinyanjui wa Nakuru kwa upande wake alitumia shilingi milioni 64 kukarabati barabara za mashinani, shilingi milioni 34.6 kwa mradi wa kufanikisha mpango wa ukusanyaji kodi, shilingi milioni 34.6 kununua vifaa vya hospitali katika Hospitali ya Nakuru Level Five.