
Magavana chini ya mwamvuli wa Baraza la Magavana wanatarajiwa kuandamana kutoka Hoteli ya Intercontinental kuelekea katika Mahakama ya Juu watakakowasilisha kesi kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato wa Mwaka 2019/20.
Baadae baraza hilo ambalo linatarajiwa kuandamana na maseneta na Wawakilishi Wadi, litaelekea katika Jengo la KICC ambako watakutana na wawakilishi wa mashirika ya kijamii, lengo kuu likiwa kushinikiza kutengewa kwa fedha wanazodai na serikali kuu kupitia Mswada huo wa Ugavi wa Mapato. Wylcif Wangamati ni Gavana wa Bungoma.
Kwa mujibu wa Seneta wa Nandi, Samson Cherargei mbali na suala la ugavi wa mapato, maseneta pia watakuwa wakitaka ufafanuzi kuhusu miswada 21 iliyopitishwa katika Bunge la Kitaifa pasi na kuhusishwa kwa Bunge la Seneti. Ikumbukwe kuwa tayari Naibu wa Rais, William Ruto aliwashauri magavana na maseneta kutoelekea mahakamani na badala yake kuzungumza.
Haya yanajiri wakati ambapo mabunge hayo mawili yamekuwa yakivutana kuhusu kiwango cha fedha zinazofaa kutengewa magatuzi baada ya wabunge kushikilia pendekezo la shilingi bilioni 316 na maseneta kupendekeza bilioni 327 hali ambayo haijaafikiwa kufikia sasa. Aden Duale ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.
Waziri wa Elimu Prof George Magoha leo anatarajiwa kuzindua misururu ya mijadala kuhusu Mtalaa wa Umilisi ambao umeanza kutekelezwa katika shule zote nchini.
Mijadala itazinduliwa katika maeneo manane kwa wakati mmoja huku Wakenya wakitakiwa kuwasilisha maoni yao kuhusu utekelezwaji wake.
Magoha ataongoza shughuli katika Kaunti ya Nakuru ambapo pia atatoa ripoti ya utafiti uliofanywa na Baraza la Mitihani Nchini KNEC kuhusu mbinu za kuwatathmini wanafunzi chini ya mtalaa huo.
Maafisa wengine watakaoongoza uzinduzi katika maeneo mengine saba ni Collete Suda ambaye atakuwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu, Katibu Alfred Cheruiyot atakayekuwa Shule ya Upili ya Kakamega, Belio Kipsang atakyekuwa Moi Complex Nyeri, Kevit Desai atakayekuwa Kangaru Embu, Elyas Mbai atakyekuwa Gariisa na Afisa Mkuu Mtwendaji wa TSC, Nancy Macharia ambaye atakuwa Mombasa