array(0) { } Radio Maisha | Matiang'i apuuza madai ya mgawanyiko katika Baraza la Mawaziri

Matiang'i apuuza madai ya mgawanyiko katika Baraza la Mawaziri

Matiang'i apuuza madai ya mgawanyiko katika Baraza la Mawaziri

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i amepuuza madai kwamba kuna mgawanyiko katika Baraza la Mawaziri hasa baada ya baadhi yao kuhusishwa na madai ya kuwepo kwa njama ya kumuua Naibu wa Rais, William Ruto.

Akizungumza katika hafla ya mazishi ya nyanyaye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Joe Mucheru katika eneo la Kirichu Kaunti ya Nyeri, Waziri Matiang'i amesema madai hayo hayana ukweli na yanalenga kuhujumu utendakazi wao serikalini.

Aidha Waziri wa Uchukuzi, James Macharia amesisitiza kwamba wataendeleza mikutano yao katika Hoteli ya La-Mada kupanga miradi ya maendeleo licha ya tetesi kwamba Rais Uhuru Kenyatta aliwataka kusitisha mikutano hiyo mara moja.

Wakati uo huo, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen amewashauri viongozi wa Chama cha Jubilee kuhubiri amani badala ya kueneza siasa za chuki chamani.

Kauli yake imetiliwa mkazo na Mbunge wa Nyeri Mjini, Wambugu Ngunjiri ambaye amewasihi viongozi wa Jubilee kukoma kueneza siasa zilizopitwa na wakati na zinazolenga kulemaza miradi ya maendeleo serikalini.