array(0) { } Radio Maisha | Wizara ya Elimu yatoa makataa kwa wanafunzi wa darasa la nane.

Wizara ya Elimu yatoa makataa kwa wanafunzi wa darasa la nane.

Wizara ya Elimu yatoa makataa kwa wanafunzi wa darasa la nane.

Wizara ya Elimu imetoa makataa ya hadi Julai tarehe thelathini na moja kwa watahiniwa wa darasa la nane kuthibitisha shule za upili walizochagua kujiunga nazo, tofauti na awali ambapo waliruhusiwa kufanya hivyo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa KCPE.

Katibu katika wizara hiyo, Belio Kipsang  amesema serikali itahakikisha kwamba watahiniwa hao wanapata angalau shule moja miongoni mwa zile walizozichagua. Miongoni mwa shule wanazozichagua, nne ni za kitaifa, nne za nje ya kaunti na mbili za kaunti kisha moja ya kutwa.

Belio aidha amewashauri walimu kukamilisha silabasi mapema ili kuwapa watahiniwa muda wa kutosha kudurusu. Amesema kuanzia sasa, maafisa wa elimu watakuwa wakitembelea shule mbalimbali kutathmini maandalizi ya watahiniwa.

Akizungumza katika Ukumbi wa KICC alipokutana na washikadau katika sekta ya elimu, Waziri wa Elimu Profesa, George Magoha amewaagiza maafisa wa Baraza la Mitihani, KNEC kufungua mfumo wa usajili, NEMIS ili kuwaruhusu watahiniwa wa darasa la nane mwaka huu kubadili shule za upili walizochagua na kuzichagua nyingine wanazozipendelea. 

Kwa mujibu wa Magoha, baadhi ya wanafunzi wanaokosa kupata barua za shule za upili baada ya mitihani ni kutokana na ushauri usiofaa wanaopewa na wazazi, vilevile walimu.

Magoha aidha amesema ushirikiano mzuri miongoni mwa washikadau hao utaboresha matokeo ya mitihani ya kitaifa mwaka huu.

Hata hivyo, Magoha amewaonya viongozi wa Kaskazini Mashariki ya nchi kukoma kuingiza siasa suala la elimu na badala yake kuunga mkono mikakati inayowekwa na serikali.

Mitihani hiyo inatarajiwa kuanza tarehe 29 hadi 31 Oktoba kwa watahiniwa wa KCPE na Novemba tarehe mosi hadi 27 kwa wale wa kidato cha nne, KCSE.