array(0) { } Radio Maisha | Wachina wasiokuwa na kibali kufurushwa mara moja; asema Waziri Matiang'i

Wachina wasiokuwa na kibali kufurushwa mara moja; asema Waziri Matiang'i

Wachina wasiokuwa na kibali kufurushwa mara moja; asema Waziri Matiang'i

Ikiwa ni njia mojawapo ya kukabili hali ya watu kuingia nchini na kutoka bila kuzingatiza utaratibu, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi Dkt. Fred Matiang'i ametoa agizo la kufurushwa kwa watu sita raia wa nchi za kigeni wanaoendesha biashara jijini Nairobi kinyume na sheria.

Akizungumza wakati uzinduzi wa kituo cha usajili wa paspoti mjini Nakuru, Waziri Matiang'i amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi  ya watakaosafiri kwenda nje au kuja nchini bila kufuata sheria.

Wakazi wa kaunti za Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet, Baringo na Bomet wanatarajiwa kupata wepesi wa kujisajili ili kupata paspoti baada ya kulalamikia changamoto za usafiri kwenda jijini Kisumu kwa usajili huo.

Wakati uo huo, Matiang'i amewakosoa viongozi wa eneo la Bonde la Ufa wakiongozwa na Gavana wa Turkana, Josephat Nanok na Alex Tolgos wa Elgeyo Marakwet, kwa kuikosoa serikali baada ya kuwapokonya bunduki Polisi wa Akiba, NPR.

Matiang'i amewalaumu viongozi hao kwa kuingiza siasa suala la oparesheni ya serikali katika kuvikabili visa vya uhalifu kutokana na ongezeko la mauaji ya watu na wizi wa mifugo katika maeneo hayo.

Akirejelea matamshi ya baadhi ya wanasiasa akiwamo Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri kuhusu siasa za mwaka wa 2022, Matiang'i amewashauri viongozi hao kukoma kutoa kauli zinazoweza kuibua chuki na migawanyiko miongoni mwa wananchi.