array(0) { } Radio Maisha | Hofu imetanda KRA kufuatia uteuzi wa James Mburu kuwa Kamishna Mkuu

Hofu imetanda KRA kufuatia uteuzi wa James Mburu kuwa Kamishna Mkuu

Hofu imetanda KRA kufuatia uteuzi wa James Mburu kuwa Kamishna Mkuu

Huenda baadhi ya maafisa wakuu katika Mamlaka ya Ukusanyaji Kodi, KRA wakajiuzulu kufuatia uteuzi wa James Gathii Mburu kuwa Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo.

Baadhi ya maafisa wakuu ambao hawakutaka majina yao kutajwa wameaimbia Radio Maisha kwamba awali walikuwa wamezozana na Mburu hivyo kuhofia kufutwa kazi.

Wanasema Mburu amekuwa akitumia na Idara ya Upelelezi, DCI kuwafanyia uchunguzi maafisa wa KRA wanaokwepa kulipa kodi au kushirikiana na watu wengine kukwepa kulipa kodi.

Alhamisi wiki hii, Waziri wa Fedha, Henry Rotich alichapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali jina la Mburu ili kushikilia wadhfa wa Kamishna Mkuu kwa katika kipindi cha miaka mitatu.

Mburu atakayeanza kuhudumu rasmi tarehe moja mwezi Julai mwaka huu, atachukua wadhifa huo kutoka kwa John Njiraini, ambaye muda wake wa kuhudumu umekamilika mwezi huu.

Kwa sasa, Mburu anahudumu katika KRA ambapo ni Kamishna wa Masuala ya Ujasusi katika mamlaka hiyo. Mburu alikuwa miongoni mwa watu watano waliohojiwa baada ya wadhifa huo uliotangazwa kuwa wazi Aprili mwaka huu kuwavutia watu thelathini.

Waliohojiwa ni Julius Waita Mwatu, Richard Buru Ndung’u, Andrew Kazora Okello na Duncan Otieno Onduru.

Mwaka jana, Bodi ya KRA iliongeza muda wa kuhudumu kwa mwaka mmoja kwa Njiraini kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta.