array(0) { } Radio Maisha | Uchaguzi wa Ford Kenya waendelea kote nchini

Uchaguzi wa Ford Kenya waendelea kote nchini

Uchaguzi wa Ford Kenya waendelea kote nchini

Huku kura za mashinani za chama cha Ford Kenya zikiendelea nchini, Kiongozi wa chama hicho Moses Wetangula amewashauri wanachama kuhakikisha shughuli hiyo inaendeshwa kwa amani.

Akizungumza kwenye Eneo Bunge la Kabuchai Kaunti ya Bungoma, Wetangula amesema kuwa tayari shughuli hiyo imetekelezwa katika kaunti 38 nchini na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni kabla ya kongamano la kitaifa kufanyika Agosti mwaka huu.

Kadhalika amesema kuwa jopo linalochunguza uchaguzi uliobatilishwa wa Kaunti ya Trans Nzoia linatarajiwa kutoa ripoti wiki ijayo na kutoa suluhu ikizingatiwa kuwa kaunti hiyo ni ngome kuu ya chama cha Ford Kenya.

Mwezi uliopita, Ford Kenya ilibuni jopo litakalochunguza jinsi shughuli ya uchaguzi wa viongozi mashinani ilivyofanyika katika Kaunti ya Trans Nzoia.  Hatua hii ilijiri baada ya malalamishi kuibuka kuhusu jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika huku ikidaiwa kuwa haukuwapo uwazi.

Jopo hilo linaloongozwa na Mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi limetakiwa kufanya uchunguzi kuhusu uchaguzi huo na kutoa suluhu ya jinsi tatizo hilo litakavyoshughulikiwa.