array(0) { } Radio Maisha | Maseneta waishtumu Idara ya Polisi kwa kuwadhalilisha viongozi

Maseneta waishtumu Idara ya Polisi kwa kuwadhalilisha viongozi

Maseneta waishtumu Idara ya Polisi kwa kuwadhalilisha viongozi

Kamati ya Sheria katika Bunge la Seneti imeikosoa Idara ya Polisi kwa madai ya kuruhusu kutumiwa vibaya na baadhi ya viongozi serikalini katika kuwahujumu mahasimu wao wa kisiasa.

Mwenyekiiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, amesema Idara ya Upelelezi DCI na ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma DPP, zinatumiwa kwa ajenda za binafsi badala ya kudumisha majukumu yao ya kikatiba.

Cherargei ameishumu DCI kwa kuwanasa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa na Mbunge wa Matungu Justus Murunga; ambao walizuiliwa kwa zaidi ya siku mbili kisha kuachiliwa kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kuwahusisha na mauaji ya Matungu.

Hata hivyo seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Juniour, amewashauri Maafisa wa Upelelezi kuchunguza uwezekano wa itikadi kali ya kafara katika mauaji hayo ya Matungu.

Kwa upande wake Kiongozi wa Wachache James Orengo, amesema uongozi wa kiimla umeanza kujitokeza katika utendakazi wa polisi hali ambayo inakiuka mwongozo wa utumishi kwa umma kwa sasa.

Hata hivyo Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen amewasihi maseneta wenzake kuepuka desturi ya kuwakosoa polisi kwa misingi ya kuwatetea wandani wao wa kisiasa. Amesema hata wananchi wa kawaida wanakumbana na via vya unyanyasaji wa polisi hali ambayo inafaaa kukashifiwa.

Maseneta hao kwa kauli moja wameitaka Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi IPOA, kufanya uchunguzi wake kwa haraka ili kuwakabili maafisa wa polisi wanaokiuka haki za washukiwa.

Haya yanajiri huku idadi ya waliouliwa na wahalifu katika eneo la Matungu ikifika ishirini na saba, Kisa cha hivi punde kikiwa cha jana ambapo mtoto Malik Moi wa miaka saba aliuliwa kisha mshukiwa wa mauaji yake kunaswa na maafisa wa GSU.