array(0) { } Radio Maisha | Rais mstaafu Moi asajiliwa kwa Huduma Namba

Rais mstaafu Moi asajiliwa kwa Huduma Namba

Rais mstaafu Moi asajiliwa kwa Huduma Namba

Na Beatrice Maganga,

NAIROBI, KENYA, Rais Mstaafu, Daniel Arap Moi amejiunga na mamilioni ya watu katika usajili wa Huduma Namba.

Mzee Moi amesajiliwa katika boma lake la Kabarnet Gardens, jijini Nairobi ambapo Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano, Joe Mucheru alihudhuria shughuli yenyewe. Aidha, mwanawe ambaye ni Seneta wa Baringo, Gideon Moi alikuwapo wakati wa usajili huo.

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i, amesema kufikia sasa idadi kubwa ya watu wamesajiliwa na huenda idadi hiyo imefikia watu milioni thelathini na tano.

Akizungumza jijini Nairobi, Matiang'i hata hivyo amesikitikia idadi kubwa ya watu ambao wamejitokeza wakati wa mwisho kusajiliwa ikizingatiwa serikali haitaongeza muda wa usajili.

Amesisitiza kwamba shughuli yenyewe itakamilika hapo kesho kwani hakuna fedha za kutosha kuongeza muda wa usajili huo, huku akiwahakikishia wote ambao wamefika vituoni kusajiliwa kuwa watahudumiwa. Waziri Matiang'i amesema ripoti kuhusu usajili wenyewe itawasilishwa Jumamosi kwa Rais Uhuru Kenyatta.