array(0) { } Radio Maisha | Makala Maalumu; Jamii ya Sabaot yahisi kuhujumiwa kwa Mipaka.

Makala Maalumu; Jamii ya Sabaot yahisi kuhujumiwa kwa Mipaka.

Makala Maalumu; Jamii ya Sabaot yahisi kuhujumiwa kwa Mipaka.

 

Na Esther Kirong'

Huku mswada uliowasilishwa katika Bunge la Seneti kutaka Eneo Bunge la Mlima Elgon kujitenga na Kaunti ya Bungoma kisha kujiunga na Kaunti ya Trans Nzoia ukisubiriwa kujadiliwa, hisia mbalimbali zinaanza kuibuliwa huku baadhi ya viongozi wakipinga waziwazi mswada huo.

Aidha wakazi wa eneo hilo wanasema wakati umefika kwa eneo la Mlima Elgon kujitenga na Bungoma, wakidai kwamba wametengwa kimaendeleo na hata nyadhifa za uongozi. 

Licha ya ugatuzi, wakazi wa Mlima Elgon wanasema kwamba hawajanufaika; wanalalamikia miundo msingi duni kwani wanalazimika kutembea takriban kilomita 50 ili kufika mjini Bungoma kuliko na makao makuu ya serikali ya Kaunti ya Bungoma ili kuhudumiwa.

Aidha, hospitali mbili pekee wanayojivunia ni za Kapsokwony na Kopsiro ila hazina vifaa vya kisasa vya matibabu. Aidha, hakuna shule ya kujivunia; nyingi ziko nje ya Malima Elgon mfano Friends School Kamusinga, Chesamis, St. Lukes Kimili na kadhalika, hali inayowalazimu wakazi kuwapeleka wanao mbali kutafuta masomo.

Pia historia inaonesha kwamba kabla ya Wakoloni, jamii ya Sabaot ilizagaa hadi Trans Nzoia, na ndiyo maana ingali inahisi kwamba eneo la Mlima Elgon inafaa kuwa kwenye Kaunti ya Trans Nzoia wala si Bungoma.

Kaunti ya Bungoma ina jumla ya watu milioni 1.4 miongoni mwao ni Jamii ya Bukusu ikiongoza kwa watu zaidi ya milioni moja, jamii ya Sabaot ikiwa watu zaidi ya laki mbili unusu huku jamii ya Iteso ikiwa na watu wasiozidi elfu hamsini.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka wa 2009, idadi ya watu kwenye Kaunti ya Trans Nzoia ni elfu 818, 757 huku jamii ya Sabaot ikiwa na asilimia 29.3 ya watu kwenye kaunti hiyo, ambayo baada ya ugavi na ununuaji wa ardhi baada ya ukoloni, sasa ni makazi ya watu wa jamii mbalimbali nchini. Kwa jumla, watu wa jamii ya Sabaot ni nusu milioni katika kaunti zote mbili ila inahisi kutengwa kimaendeleo, ajira, elimu na kadhalika.

Jamii ya Sabaot, zamani ikiitwa Elgon Maasai, inaishi kando kando ya Mlima Elgon. Wasabaot walikuwa wafugaji ila wakalazimika kuingilia ukulima kutokana na kupungua kwa ardhi za kuwalishia mifugo. Licha ya eneo hili kuwa lenye rutuba ya hali ya juu, kuzalisha mazao mengi shambani usafirishaji hadi sokoni umekuwa jinamizi…wanalazimika kusafiri mwendo mrefu huku mazao yenyewe yakioza njiani.

Kwa ujumla, jamii ya Sabaot inachangia zaidi ya asilimia 70 ya uchumi wa Bungoma hasa ikizingatiwa kaunti hiyo inategemea Mlima Elgon katika uzalishaji wa chakula, sekta ya biashara vilevile utalii.

Licha ya kwamba kuna matumaini kutokana na utiaji lamu kutoka Kamukuywa – Kaptama –Kapsokwony – Kamuneru- Kapkateny, barabara kuu ya Kapsokwony - Kimilili ambayo ni muhimu mno kwa wakazi hao, ungali umesahaulika. Licha ya vivutio vya kitalii hasa katika Msitu wa Mlima Elgon wenye wanyamapori aina aina, hakuna mtalii anayezuru eneo hilo kutokana na barabara mbaya.

Hata hivyo, licha ya wakazi hao kuzungumza kwa kauli moja, baadhi wanapinga vikali suala la kujitenga na Bungoma huku wakiwasuta wenzao kwa kuwa na njama fiche. Martin Kipsoi ni Kiongozi wa Vijana.

Katika siku za hivi karibuni, wakazi wamekuwa wakilalamikia kunyanyaswa na viongozi wa kaunti hizo mbili licha ya kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi. Kulingana na viongozi wa jamii hiyo, wamenyanyaswa, wametengwa, wamedhulumiwa na sasa wanataka kujiondoa lakini vipi

Kwa sasa inasubiriwa kuona iwapo mswada uliowasilishwa katika seneti utapitishwa na kuzaa matunda kwa wakazi wa Mlima Elgon na wenzao wa Trans Nzoia.

Iwapo utapita, basi utakuwa mwamko mpya Mlima Elgon. Itakuwa mojawapo ya hatua kubwa kwa jamii hii ambayo inahisi kujiunga na wenzao Kaskazini mwa Bonde la Ufa, jamii ambayo haina cha kujivunia kwani licha ya kuwa na wasomi, serikali haijakuwa ikiwateua katika nyadhfa za serikali huku wanaoteuliwa wakiwa tu wanaojuana na watu tajika.