array(0) { } Radio Maisha | Mwili wa afisa wa Gereza la Murang'a wapatikana ukiwa na majeraha ya kisu

Mwili wa afisa wa Gereza la Murang'a wapatikana ukiwa na majeraha ya kisu

Mwili wa afisa wa Gereza la Murang'a wapatikana ukiwa na majeraha ya kisu

Afisa mmoja wa Gereza la Murang'a, amepatikana ameuliwa nyumbani kwake kwenye eneo la Kiharu. Mwili wa afisa huyo kwa jina Pauline Wangari mwenye  umri wa miaka 24 umepatikana ukiwa na majeraha kadhaa ya kisu kifuani, kichwani ya tumboni huku ukiwa tayari umeanza kuoza.

Kamanda wa Polisi kwenye Kaunti ya  Murang'a, Josphat Kinyua amesema huenda afisa huyo aliuliwa siku ya Jumatatu usiku.

Kinyua amesema harakati za kumtafuta zilianza baada ya yeye kukosa kuripoti kazini. Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa huenda aliuliwa kufuatia mzozo wa kimapenzi. Wanaomtambua mwendazake wamemtaja kuwa mtu aliyependa kujivinjari. 

Ni jana ambapo tukio tofauti la mauaji lilishuhudiwa kwenye Kaunti ya Laikipia baada ya mfanyakazi mmoja wa Shule ya Wasichana ya Njonjo Laikipia, kumdunga kwa kisu mwenzake, kabla ya kujinyonga kufuatia mzozo wa kimapenzi. George Thenya alimshambulia kwa kisu mfanyakazi mwenzake Naomi Nyambura, baada ya mzozo kati yao.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, wawili hao walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi tangu mwaka jana. Mshukiwa alijinyonga kutumia kamba alipodhania kwamba mpenzi wake alikuwa tayari amefariki dunia. Kamanda wa Polisi wa Nyahururu, Geofrey Mayek alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu kisa hicho huku mwathiriwa akiendelea kutibiwa.