array(0) { } Radio Maisha | Mwili wa Ivy Wangeci wazikwa

Mwili wa Ivy Wangeci wazikwa

Mwili wa Ivy Wangeci wazikwa

Hatimaye Ivy Wangechi mwanafunzi wa chuo Kikuu cha Moi ambaye aliuliwa na aliyekuwa mpenziwe Naftali Kinuthia kwa kukatwa kwa shoka, amezikwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Mahiga kwenye Kaunti ya Nyeri. Viongozi,  jamaa na marafiki waliofika katika hafla ya mazishi wamekishtumu kitendo hicho cha mauaji huku wakimtaka mshukiwa afunguliwe mashtaka mara moja. 

Ni siku ambayo imekuwa ya majonzi hasa baada ya Mwili wa Ivy Wangechi kuwasili katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Mahiga.

Wanafunzi aliokuwa akisoma nao, ndugu, jamaa na marafiki walijumuika ili kumpa buriani ya mwisho Wangecy, mwanafunzi wa mwaka wa 6 ambaye alitarajiwa kuhitimu kwa shahada ya Udaktari mwisho wa mwaka huu.

Akiwahutubia waombolezaji, mamaye Ivy, Winfred Wangechi amemtaja bintiye kuwa mtoto mtiifu na aliyependa masomo.

Aidha ndugu na dada zake Ivy, cheryl na Elvis wamemtaja kuwa dada wa pekee ambaye walimpenda kwa dhati.

Wanafunzi wa chuo Kikuu cha Moi waliofika kwa wingi aidha wametoa risala zao huku wakikilaani kitendo hicho cha mauaji kwa mwanafunzi mwenzao.

Kwa upande wao, viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wakiwamo Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, Moses Kuria wa Gatundu kusini, Mwakilishi wa Kike kwenye kaunti ya Murang’a Sabina Chege na viongozi wengine wameshtumu mauaji hayo huku wakiyataja kuwa ya kikatili.

Ivy Wangeci aliuliwa na Naftali Kinuthia kwa kukatwa kwa shoka nje ya Hospitali ya Rufaa ya Moi wiki mbili zilizopita, kwa madai kwamba Ivy amekuwa akimpuuuza licha ya kuwekeza kwake pakubwa, na hata alikuwa ametumia shilingi elfu 14 za kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake siku chache kabla ya mauaji hayo.

Hadi sasa, mshukiwa huyo yupo rumande akitarajiwa kufunguliwa mashtaka ya mauaji baada ya kufikishwa mahakamani na kupewa muda wa kupona kabla ya kesi kuanza rasmi.