array(0) { } Radio Maisha | ANC yatangaza kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na Rais Kenyatta

ANC yatangaza kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na Rais Kenyatta

ANC yatangaza kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na Rais Kenyatta

Viongozi wa Chama cha ANC, chake Musalia Mudavadi wametangaza kuunga mkono kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba serikali yake itafanikisha maendeleo kote nchini bila ubaguzi. Wakiwahutubia wanahabari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Nairobi, viongozi hao wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa ANC, Ayub Savula wamesema licha ya kuwa katika chama pinzani, wanaunga mkono juhudi zozote za serikali kuboresha maisha ya wananchi.

Savula aidha ameirejelea kauli ya Rais Kenyatta ya kuwaita 'washenzi ' watu wanaomshtumu kwa madai ya kutolizingatia eneo la Kati ya Nchi kimaendeleo akisema Rais anajukumu la kuwahudumiwa Wakenya wote kwa usawa bila kuyajali maeneo wanayotoka.

Wakati uo huo, amewashtumu wabunge na wanasiasa wengine wa eneo la Magharibi ya Nchi hasa walioko katika Chama cha ANC wanaodaiwa kulipwa na wanasiasa fulani kuwapigia debe kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2022 akisema wanasiasa hao wanastahili kutangaza msimamo wao kuhusu upande wanaounga mkono.

Chama hicho aidha kimempongeza Rais Kenyatta kwa kuagiza kuanza kununuliwa kwa mahindi kutoka kwa wakulima, vilevile kuidhinishwa kwa malipo ya wakulima wa miwa na kutoa wito kwa Wizara ya Fedha kufanikisha malipo hayo haraka ili wakulima wapate fedha za kuwalipia wanao karo. Beatrice Adagala ni Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Vihiga vilevile mwanachama wa ANC.