array(0) { } Radio Maisha | Rais Kenyatta awatakia Wakenya mwaka mpya wenye fanaka huku akiahidi kutimiza ahadi mbalimbali za maendeleo

Rais Kenyatta awatakia Wakenya mwaka mpya wenye fanaka huku akiahidi kutimiza ahadi mbalimbali za maendeleo

Rais Kenyatta awatakia Wakenya mwaka mpya wenye fanaka huku akiahidi kutimiza ahadi mbalimbali za maendeleo

Rais Uhuru Kenyatta ameelezea maazimio ya kufanikisha ajenda nne kuu za serikali mwaka mpya unapoanza. Katika hotuba yake kwa taifa ya kufunga mwaka akiwa jijini Mombasa, Rais Kenyatta amesema utekelezaji wa ajenda hizo ambazo ni afya bora kwa wote, utoshelezo wa chakula, kubuniwa kwa nafasi zaidi za ajira kupitia kuboreshwa kwa sekta ya viwanda na kujengwa kwa makazi yatakayokodishwa kwa bei nafuu, kutaboresha zaidi maisha ya Wakenya.

Kwa mara nyingine Rais amerejelea kujitolea kwake kukabili ufisadi huku akiwashauri wanaolenga kujiimarisha maishani kufanya hivyo kwa njia za uwazi na kujiepusha na ufisadi. Rais aliahidi  kuweka mikakati zaidi ya kutwaa mali ya umma ambayo ilitwaliwa kwa njia za ufisadi. 

Rais Kenyatta aidha amepongeza ushirikiano kati yake na Kinara wa ODM, Raila Odinga akisema uamuzi huo wa ushirikiano umekuwa wa manufaa kwa taifa na unaolenga kuzuia ghasia wakati wa uchaguzi siku za usoni.

Rais Kenyatta aidha alizipongeza serikali za kaunti kwa kujitolea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya afya, elimu, kilimo miongoni mwa miradi nyingine kulingana na maazimio ya katiba ya sasa. Wakati uo huo aliwapongeza wanajeshi wa KDF na maafisa wengine wa usalama kwa kujitolea kwao kulihudumia taifa na kuyakabili makundi ya kigaidi vilevile wahalifu.  

Huku shule zikitarajiwa kufunguliwa siku ya Alhamisi wiki hii kwa muhula wa kwanza, Rais Kenyatta ameahidi kutekelezwa kwa mfumo mpya wa elimu akisema utakuwa wa manufaa kwa wanafunzi na kizazi cha sasa katika kuwapa ujuzi wa kuwafanikisha maishani. Aidha amevitaka vyuo vikuu kudumisha hadhi yake kwa kuepusha visa vya udanganyifu katika mitihani.

Rais Kenyatta aidha ameupongeza ushirikiano ambao umekuwapo baina ya Kenya na mataifa mengine yakiwamo  Uchina,Uingereza, Marekani na Japani na kuahidi kwamba ushirikiano huo utaimarishwa zaidi mwaka huu wa 2019 ili kufanikisha maendeleo.