array(0) { } Radio Maisha | Hatimaye Taj Mall yabomolewa

Hatimaye Taj Mall yabomolewa

Hatimaye Taj Mall yabomolewa

Hatimaye shughuli ya kulibomoa Jumba la Airgate Centre awali likijulikana kuwa Taj Mall imeanza muda mfupi uliopita. Maafisa wa usalama wameimarisha doria  kuhakikisha shughuli hiyo iliyoanza mwendo wa saa kumi na mbili unusu asubuhi haitatizwi na yeyote. Ubomoaji wa jengo hilo unafanyika baada ya makataa kwa mmiliki wake kulibomoa kukamilika mwishoni wa mwezi uliopita.

Siku chache zilizopita, Mwenyekiti wa jopo maalum la kushughulikia ubomoaji huo, Moses Nyakiongora na Afisa wa Kaunti ya Nairobi, Julius Wanjau, walisema shughuli ya kulibomoa jengo hilo ambalo limejengwa eneo lililotengewa barabara ingeanza baada ya kukamilisha kabisa ubomoaji wa majumba mengine kama vile Southend Mall.

Ikumbukwe mmiliki wa jumba hilo la  Airgate Centre, Ramesh Gorassia alikataa katakata kulibomoa mwenyewe akisisitiza alifuata taratibu zote za kisheria. Tayari wafanyabiashara katika jengo hilo waliondoa bidhaa zao baada ya kufahamishwa kuhusu notisi ya ubomoaji.